Manchester City na Arsenal wanatarajiwa kuvaana katika Ligi Kuu ya Uingereza, siku ya Septemba 22, 2024.
Safu ya ulinzi ya Arsenal inasifika kwa kuwa na safu imara ya ulinzi huku ikiwa ikiruhusu bao moja tu katika mchezo dhidi ya Brighton, itakuwa na kibarua kigumu kumdhibiti mshambuliaji mwenye uchu wa kufunga, Erling Haaland.
Haaland anaongoza orodha ya wafungaji kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, akiwa ameshatupia mabao tisa msimu huu.
"Ni timu nyingine isiyotabirika kwani ina ulinzi imara," alisema kocha wa City Pep Guardiola. "Hawaruhusu nafasi, hawaruhusu mabao. Katika nyanja nyingi wanadhibiti kila kitu.
"Ilikuwa changamoto kubwa kwa taji misimu miwili iliyopita, wapo na watakuwepo kwa miaka mingi kwa sababu waliunda kikosi kizuri na kichanga ."
City ndio timu pekee iliyo na alama 12 kamili hadi sasa, lakini Arsenal iliyopata sara moja, inaendelea kuifukuzia Manchester City mgongoni, huku ikiwa imetofautiana nayo kwa alama mbili, baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Spurs kwenye 'dabi' ya kaskazini mwa London, wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, 'washika bunduki' hao watamkosa nahodha Martin Odegaard kwa mara nyingine tena kutokana na kuwa na jeraha la kifundo cha mguu huku Declan Rice akirejea uwanjani baada ya kumaliza kifungo chake cha mechi moja.
Kwa upande wao, City watamkosa kiungo mchezeshaji wao, Kevin De Bruyne ambaye alipata majeraha baada ya sare ya City na Inter Milan, katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mbali na hayo, Kocha wa Tottenham Ange Postecoglou atahitaji ushindi wakati timu yake itakapoikaribisha Brentford huku Liverpool wakipata nafasi ya kutafakari kwa A.F.C. Bournemouth.