United ilisalimu uongozi wa mabao mawili na kuishia sare ya 3-3 na Galatasaray huko Istanbul/ Photo: Reuters

Manchester United wanakabiliwa na hatari ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa katika hatua ya makundi.

Hii ni baada ya kusalimu uongozi wa mabao mawili na kuishia sare ya 3-3 na Galatasaray huko Istanbul Jumatano.

United, mabingwa mara tatu wa Ulaya walihitaji ushindi nchini Uturuki, dhidi ya wapinzani hao walioilaza Old Trafford mwezi Oktoba, ili kuweza kufuzu kwa raundi za mtoano mikononi mwao.

Timu hiyo ya Erik ten Hag ilionekana kudhibiti mechi baada ya Alejandro Garnacho kupachika goli la kwanza kabla ya Bruno Fernandes kuongeza la pili dakika 18.

Hakim Ziyech aliirudisha Galatasaray bao moja kupitia mkwaju wa ikabu, kabla ya Scott McTominay kuzidisha uongozi wa wageni wa mabao mawili mwanzoni mwa nusu ya pili.

Hata Hivyo, Galatasaray walifufua tena matumaini yao kupitia mkwaju wa Ziyech baada ya kipa wa United Andre Onana kutapatapa langoni, kabla ya wenyeji kusawazisha kupitia kombora la dakika ya 71 la Kerem Akturkoglu.

Arsenal na PSV Eindhoven walijihakikishia nafasi zao timu 16 ya mwisho na kujiunga na Atlético de Madrid, Barcelona, Bayern Munich, Dortmund, Inter, Lazio, Leipzig, Man City, PSV, Real Madrid, Real Sociedad ambao walifuzu kuingia hatua ya muondoano.

Mechi za raundi ya 16 zitafanyika kati ya tarehe 13/14 na 20/21 Februari 2024.

TRT Afrika na mashirika ya habari