Timu ya soka kutoka Uingereza, Manchester City waliifunga Tottenham Hotspur 2-0 Jumanne na kupanda kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza, na kuweka hatua kwa mechi ya kusisimua ya mwisho dhidi ya West Ham United Jumapili.
Mshambuliaji Erling Haaland alifunga bao la kwanza la City katika dakika ya 51, na bao la pili kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya kwanza ya dakika 10 zilizoongezwa mwishoni mwa kipindi cha pili.
Baada ya kucheza mechi 37 katika msimu wa 2023/24, City sasa wana pointi 88, mbili zaidi ya wapinzania wao wakubwa kutoka London, Arsenal, walio katika nafasi ya pili, ambao pia wamecheza idadi sawa ya michezo.
Arsenal watakutana na Everton katika Uwanja wa Emirates kwenye mechi yao ya mwisho Jumapili.
Taji la nne mfululizo kwa City?
City, ambao watacheza katika Uwanja wa Etihad dhidi ya West Ham Jumapili, wanatafuta kuwa klabu ya kwanza katika historia kushinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Hata hivyo, matumaini hayajapotea kwa Arsenal kwani misukosuko ya siku ya mwisho inaweza kuwapa taji lao la kwanza la Ligi Kuu ya Uingereza baada ya miaka 20.