Faith Kipyegon akisherehekea ushindi wake na kuweka rekodi mpya ya dunia katika fainali ya mita 1,500 kwa wanawake,  / Picha: Reuters

Malkia mara mbili wa Olimpiki anayeshikilia rekodi za dunia mita 1,500 na mita 5,000, Faith Kipyegon, anatarajiwa kuweka rekodi zaidi atakapoingia uwanja wa Louis II kwenye mbio za Maili ya Wanawake, umbali alioshiriki mara ya mwisho mnamo 2016 mjini Oslo, Norway.

Faith Kipyegon, ambaye alionyesha uhodari wake wakati wa mbio za Wanda Diamond League, atajirusha uwanjani Monaco akiwa mmoja wa mastaa wa riadha duniani watakaowania sifa kwenye vitengo tofauti.

"Hapo awali nilikuwa nimepanga kukimbia mbio za 1500m lakini sasa nimechagua kukimbia maili huko Monaco Ijumaa hii," Kipyegon alisema.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, anavizia rekodi ya mkimbiaji wa Uholanzi Sifan Hassan ya muda wa dakika 4:12.33, iliyowekwa mnamo 2019.

Kipyegon atapambana na mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki ya mita 1500 Laura Muir wa Uingereza, Freweyni Hailu mshindi wa medali ya fedha ya Ndani ya Dunia na Habitam Alemu mshindi wa nishani ya shaba Afrika 2018.

“Jambo zuri ni kwamba pointi nitakazopata katika kinyang’anyiro hicho bado zitaelekezwa kwa kile ambacho tayari nimejikusanyia katika mbio za 1500m,” Kipyegon alisema.

Sasa anaelekeza umakini wake kwenye maili, ambapo ubora wake wa kibinafsi wa 4:16.71 uliwekwa mnamo 2015.

TRT Afrika