Malkia hao wa Kenya wametawazwa ubingwa wa Afrika baada ya miaka nane, na kushinda taji lao la 10 kufuatia ushindi dhidi ya Misri kwenye fainali kupitia seti tatu ya 3-0 (25-22, 25-20, 25-14).
Kufuatia ubingwa huo, Malkia hao wa Kenya, pia wamejikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 na pia kuruka kutoka nafasi ya 30 hadi 22 katika jedwali ya orodha mpya ya timu bora ya voliboli kwa wanawake duniani kutoka FIVB.
Kenya ililipiza kisasi dhidi ya wenyeji na bingwa mtetezi, Cameroon kwa kuizaba 3-1 (25-27, 25-14, 25-11, 25-18) katika hatua ya nusu fainali.
Wenyeji Cameroon walichukua medali ya shaba baada ya kuishinda Rwanda 1-3.
Pongezi kutoka Rais wa Kenya William Ruto.
Wachezaji bora wa Mashindano
Nahodha wa timu ya Kenya, Mercy Moim alitunukiwa kuwa mpokeaji Bora wa Kombe la Mataifa bora ya Voliboli ya Afrika kwa Wanawake CAVB 2023.
Emmaculate Nekesa aliyejaza viatu vya gwiji Jane Wacu, alitwaa tuzo ya mpiga pasi bora 'setter' huku Sharon Chepchumba maarufu "CHUMBA" ambaye aliwatesa wapinzani kwenye michuano hiyo kupitia mashambulizi yake makali uwanjani, ametajwa kuwa Mchezaji bora wa Kombe la Mataifa bora ya Voliboli ya Afrika kwa Wanawake CAVB 2023.
Kwa sasa Kenya inatazamia kwa hamu Michezo ya Afrika ya 2024 nchini Ghana na Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 huku ikiendelea na sherehe ya kufurahia taji la Malkia wa Afrika.