Intermilan yatinga fainali ya kombe la klabu bingwa ulaya Picha: Reuters.

Intermilan yatinga fainali ya kombe la klabu bingwa ulaya katika mchuano utakao fanyika Istanbul Uturuki baada ya kuitwanga AC Milan bao moja kwa bila hii leo katika mkondo wa pili wa nusu fainali ya klabu bingwa Ulaya.

Katika dakika ya sabini na moja(71) ya kipindi cha pili cha nusu fainali , kiungo matata wa Inter Milan Lautaro Martinez na Romelu Lukaku walipeana pasi katika eneo la hatari la Milan.

Martinez kisha akasogea karibu na lango na kupiga shuti la chini, kali na kwa ustadi lililompita kipa wa Milan Mike Maignan kwenye lango na kutikisa wavu.

Safu ya ulinzi ya Milan iliruhusu washambuliaji wa Inter kupokea miguso mingi sana, na mlinda mlango wao pia alikuwa duni. Maignan hataridhika na matokeo licha ya juhudi zake za kuwakomboa mara kadhaa Milan katika mechi hii.

Wiki iliyopita, Inter ilitawala kabisa mkondo wa ufunguzi wa nusu fainali, kwa kuwashinda wapinzani wao 2-0.

Huku wakijaribu kufika fainali ya shindano hilo kwa mara ya kwanza tangu walipotwaa kombe hilo mwaka 2010, Inter wako kwenye mfululizo wa kushinda mechi saba katika mashindano yote.

Macho yote sasa yanaelekezwa katika mkondo wa pili wa nusu fainali ya pili baina ya mahasidi wa jadi Real Madrid na Manchester City katika mchezo mkubwa zaidi wa soka barani Ulaya. Mshindi baina ya timu hizo mbili atachuna na Inter Milan kwenye fainali itakayo andaliwa katika jiji la Istanbul nchini uturuki.

Inter ilistahili kusonga mbele kwa sababu walikuwa timu bora katika nusu fainali zote mbili. Je, wanaweza kuinua kombe kwa mara nyingine tena?

TRT Afrika