Mabingwa watetezi Italia wametupwa nje ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya (EURO 2024) baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Uswisi.
Matokeo ya mchezo huo, uliofanyika Juni 29, katika uwanja wa Olympiastadion, mjini Berlin nchini Ujerumani, unaifanya Italia, inayofundishwa na Luciano Spalleti, kuwa timu ya kwanza kuyaaga mashindano hayo makubwa barani Ulaya katika hatua ya mtoano.
Uswisi, timu isiyopewa nafasi ya kufika mbali katika michuano hiyo mikubwa barani Ulaya, ilifunga bao lake la kwanza kupitia kwa Remo Freuler, katika dakika ya 37 ya mchezo, ndani ya kipindi cha kwanza.
Hadi timu zinaingia mapumziko, ubao wa matokeo ulisomeka 1-0, kwa faida ya Uswisi.
Mtanange huo, ulishuhudia Uswisi ikitawala zaidi katika umiliki wa mpira, idadi ya pasi na mashuti golini, dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Ulaya.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Italia walishangazwa na bao la mapema na la kushtukiza, lililofungwa na Ruben Vargas, baada ya kuachia shuti kali, nje kidogo ya eneo la adhabu, na kumuacha kipa tegemeo wa Italia, Gianluigi Donnarumma akichupa bila mafanikio yoyote.
Matokeo hayo yanaifanya Uswisi kusonga mbele kuelekea hatua ya robo fainali na vile vile kuondoa mkosi wa miaka 31 wa kufanya vibaya dhidi ya Italia.