Ni Jurgen Klopp VS Mikel Arteta Anfield. / Picha: AFP

Arsenal inaingia mechi hii ikiwa juu ya meza ya Ligi kuu ikiwa na pointi 39 baada ya mechi 17, pointi moja mbele ya Liverpool na tano zaidi ya Manchester City, iliyokuwa ikishiriki Kombe la Dunia kwa Vilabu nchini Saudi Arabia.

Wenyeji Liverpool wanaingia mechi hii bila kufungwa Anfield katika ligi kuu nchini humo tangu Oktoba 2022.

Viongozi wa ligi Arsenal wanaamini kuwa ushindi wao wa kwanza huko Anfield tangu Septemba 2012, Arteta bado akiichezea Arsenal, unaweza kuwamotisha katika azimio lao la kutwaa ligi msimu huu.

Liverpool itaingia mechi hiyo bila huduma za Alexis Mac Allister na Diogo Jota wanaouguza majeraha.

Hata hivyo, The Reds wanajigamba kuelekea mchuano huo kwani hawajawahi kupoteza katika mechi zao 10 za mwisho za Ligi kuu dhidi ya Arsenal, huku wakishinda mechi saba kati ya hizo.

Lakini upande wa Arsenal, unaoongozwa na Mikel Arteta uko kwenye fomu nzuri ya ushindi katika mechi tano kati ya sita ilizocheza hivi karibuni kwenye ligi.

Kiungo wa England, Declan Rice, aliyesainiwa na Arsenal kwa kitita kilichovunja rekodi alipojiunga nao kutoka West ham katika msimu wa joto, amewapa Gunners msukumo mzuri na kudhihirisha ada ya pauni milioni 100 iliyotumika kumsajili.

Liverpool ilikabwa sare ya 0-0 na Manchester United mwishoni mwa wiki iliyopita na kukosa fursa ya kukwea juu lakini hawajapoteza nyumbani kwenye ligi kwa zaidi ya mwaka mmoja, ingawa mnamo Jumatano, kocha wake Jurgen Klopp aliwaonya mashabiki juu ya kuridhika, huku akiwashutumu kwa kuwa kimya sana.

TRT Afrika na mashirika ya habari