Baada ya mojawapo ya barabara za mji wa Rome, Italia kupewa jina lake Abebe Bikila, sasa mwanariadha huyo amewekewa kumbukumbu ya heshima mjini humo. Shule, viwanja vya michezo na hata mojawapo ya tuzo za riadha katika New York Marathon zimepewa jina lake.
Lakini ni kwa nini?
Uwepo wa kumbukumbu ya Abebe katika mji mkuu wa Italia, taifa lililovamia Ethiopia, limeonekana kuwa historia ya aina yake.
Abebe aliingia kwenye vitabu vya historia baada ya kuweka rekodi ya dunia ya mbio za masafa marefu za Olimpiki Rome, 1960, kwa kukimbia bila viatu licha ya kudharauliwa na wanariadha wengine kwa kutokuwa na viatu.
Aidha, mbio hizo zilifanyika usiku huku chanzo za mwangaza zikiwa ni taa zilizowashwa na wanajeshi wa Italia wakiwa wameshikilia mienge kando ya barabara.
Ingawa kabla ya hapo, hakuna mtu nje ya Ethiopia aliyesikia habari za Bikila alipowasili kwenye mashindano, hajawahi kusahaulika tangu uhodari wake wa Olimpiki wa rekodi bora zaidi ulimwenguni.
Abebe alikuwa mshindi wa kwanza wa medali ya dhahabu ya Olimpiki kwa Ethiopia na Afrika ikiwa pia ni dhahabu ya kwanza ya Olimpiki kwa Mwafrika mweusi duniani. Aidha, amesalia kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki akikimbia bila viatu.
Abebe Bikila ni chanzo cha fahari ya taifa. Ni mwanariadha wa kipekee aliyeinua hadhi ya Ethiopia hadi kujulikana kwenye jukwaa la dunia na kufungua milango kwa wanariadha wengi wa Kiafrika. Anasalia kuwa ishara ya kipekee ya uvumilivu na kutoshindwa.
Abebe aliandika historia zaidi kwa kuwa mwanariadha pekee aliyeshinda medali mbili za dhahabu za marathoni zikifuatana alipohifadhi taji la mbio za masafa marefu za Olimpiki huko Tokyo 1964.
Abebe Bikila alizaliwa nchini Ethiopia tarehe 7 Agosti 1932, na kuaga dunia akiwa na umri wa miaka 41, Oktoba 1973, kutokana na maumivu ya muda mrefu ya ajali ya gari aliyohusika 1969. Zaidi ya watu 75,000 walijitokeza kushiriki kwenye mazishi yake.