Bingwa wa mbio za masafa marefu duniani, Kelvin Kiptum ameteuliwa kuwania tuzo ya mwanariadha bora wa kiume duniani 2023 na shirikisho la riadha duniani.
Mapema mwezi Oktoba, Kelvin Kiptum aliweka historia kwa kuwa mwanariadha wa kwanza kuvunja rekodi ya muda wa chini ya saa mbili na sekunde moja 2:01 alipokimbia kwa muda wa 2:00.35 katika mbio za Chicago marathon.
Kiptum aliweka muda uliobora zaidi kuliko rekodi ya dunia ya 2: 01: 09 iliyowekwa na mwenzake Eliud Kipchoge huko Berlin mwaka jana.
Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 23, ameteuliwa kuwania tuzo hiyo kutokana na uhodari wake mbioni ambapo ameingia kwenye orodha ya wanariadha vigogo walioweka rekodi duniani wakiwemo Mkenya Eliud Kipchoge na Kenenisa Bekele wa Ethiopia.
Uhodari wake Valencia mnamo Disemba, ambapo alishinda kwa muda wa 2:01:53 pamoja na mbio za London, umempiga jeki na kumwezesha kuwania tuzo ya mwanriadha bora wa kiume duniani.
Kiptum atawania tuzo hiyo dhidi ya Soufiane El Bakkali, wa Morocco ambaye ni bingwa wa mbio za mita 3000m kuruka viunzi na maji, Karsten Warholm wa Norway, Pierre LePage wa Canada, Noah Lyles wa Marekani, Alvaro Martin wa Marekani, Miltiadis Tentoglou wa Ugiriki, Neeraj Chopra wa India, Ryan Crouser wa Marekani, na Mondo Duplantis wa Sweden.