Polisi wa Brazil wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo./ Picha : Ukurasa wa Facebook klabu ya  Grêmio Esportivo Anápolis

Kipa mmoja wa klabu nchini Brazil alipigwa risasi ya mpira na afisa wa polisi.

Tukio hilo lililotokea tarehe 10 Julai 2024 wakati wa mechi ya ligi daraja la pili kati ya Gremio Anapolis na Centro Oeste.

Centro Oeste ilikuwa imeshinda mechi hiyo 2-1 kabla ya kutokea mzozo, kulingana na gazeti la Brazil Globo.

Afisa wa polisi alionekana akimpiga risasi ya mpira kipa wa Gremio Anapolis, Ramon Souza kufuatia mzozo huo.

Souza aliumizwa paja lake kwa risasi za mpira kutoka kwa polisi aliyefyatua kwa karibu sana , na kusababisha majeraha mabaya. Alipewa huduma ya kwanza uwanjani na kisha kuhamishiwa hospitali kwa gari la wagonjwa.

Kwenye mtandao wa Facebook, Klabu ya Gremio ilithibitisha kisa hicho na kusema watachukua hatua zinazohitajika ili aliyehusika aadhibiwe.

"Kitendo cha kutisha, kisichoaminika na cha uhalifu kutoka kwa mtu ambaye alipaswa kukuza usalama wa watu uwanjani. Tukio hili la vurugu na la kuchukiza halitasahaulika kamwe," Gremio iliandika.

Gremio pia ilisema kuwa kipa Souza alipata huduma ya kwanza kwa wakati, hivyo hakupata maambukizi. Jeraha hilo halihatarishi maisha na anaendelea vizuri.

Polisi wa Brazil wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

TRT Afrika