Bayindir aliokoa mikwaju miwili ya penati katika mechi yao ya raundi ya tatu dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Arsenal.
Kipa huyu aliokoa penati moja ya mchezaji Martin Odegaard wa Arsenal katika dakika ya 72 na kuwapa matumaini klabu yake ya Manchester United.
Baadaye, wakati wa maamuzi kupitia mikwaju ya penati akaokoa mkwaju uliopigwa na Kai Havertz. Hatua hii inamfanya kuwa mlinda mlango wa kwanza wa ligi kuu ya England kuokoa penati mbili. moja ndani ya muda wa mchezo na nyingine kwa mikwaju ya penati katika mechi ya kombe la FA tangu msimu wa 2013-14.
Altay Bayindir mwenye umri wa miaka 26 alipata tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo kutokana na umahiri wake langoni.
Alijiunga na Manchester United 2023 kwa mkataba wa miaka minne. Anakuwa mchezaji wa kwanza raia wa Uturuki kujiunga na klabu hiyo ya ligi kuu ya England.
Kabla ya kuelekea Uingereza alicheza katika vilabu mbali mbali nchini Uturuki ikiwemo timu ya Fenerbahce. Alicheza pia katika timu ya taifa ya U-20
2020 aliitwa kwenye timu ya taifa ya Uturuki, na 2021 alipata fursa ya kucheza katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Azerbaijan.
Kuweka kwake historia katika kombe la FA na kuivusha timu yake hadi hatua nyingine, kunamfanya awe golikipa wa kutegemewa na klabu yake ya Manchester United.