Mijadala mizito imetawala mitandao ya kijamii hasa wakati Kenya ikijiandaa kuwa mwenyeji wa droo ya michuano ya CHAN 2024 siku ya Januari 15.
Timu zitapangwa katika makundi kulingana na matokeo ya makala tatu za michezo hiyo iliyopita (2022,2020 na 2018).
Kenya, Uganda na Tanzania wanaandaa michuano hiyo kwa pamoja, huku wakijiandaa kuwa wenyeji wa michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) mwaka 2027.
Hata hivyo, siku ya Januari 14, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), lilitangaza kuahirisha michuano ya CHAN 2024 kutoka mwezi Februari hadi mwezi Agosti 2025, ikiweka wazi kuwa miundombinu katika nchi hizo, bado haikidhi matakwa na vigezo vya kuandaa mashindano hayo, ambayo ni maalumu kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani barani Afrika.
Hatua hiyo 'imewatibua' baadhi ya wadau wa michezo kwenye mitandao ya kijamiii, huku mmoja akisema kuwa , ''Ni wazi kuwa mmoja wa waandaaji hayuko tayari''
Mwingine alidhihirisha kughadhabishwa zaidi "Michuano yote imeahirishwa kwa sababu ya baadhi ya waandaaji hawako tayari, siyo sahihi. Ipelekwe sehemu nyingine." alisema mmoja wa watumiaji wa mitandao.
Michuano hii inaonekana kama maandalizi mazuri kwa ajili ya uwenyeji wa makala ya 36 ya mashindano ya mataifa ya Afrika, AFCON 2027. Uganda, Kenya na Tanzania pia wataandaa michezo hiyo.