'Mtu Kazi' ameona kazi ikimshinda nguvu alipolazwa kifudifudi na bondia wa Uganda Moses Golola katika raundi ya tatu.
Pambano kati ya Karim Mandonga na mpinzani wake Golola liliwavutia mashabiki wengi kutokana na mikeke waliotoa wakati wa mkutano na waandishi kabla ya kukutana ulingoni.
Matani ya Golola kuwa 'Mama mdogo' - akimaanisha mandonga atalia mbele za watu, yalikuja kweli alipomwekelea 'Matoke' ya kulia, sekunde chache kabla ya kengele ya kufunga raundi ya tatu na hivyo kujihakikishai ushindi wa TKO.
Wiki moja tu iliyopita, Julai 22, Mandonga alikumbana na misukosuko mingine alipopambana na bondia Mkenya Daniel Wanyonyi, ambaye pia alimtwanga na kumrejesha nyumbani kwa kumfunga kinywa.
Wengi wamekuwa wakihoji iwapo Mandonga anajiweka hatarini kwa kufululiza mapambano moja baada ya nyingine bila mapumzikpo ya kutosha.
Kawaida mabondia hupewa angalau miezo mitatu kabla ya kupangiwa pambano nyingine, jambo ambalo Mandonga amekuwa akipuuza.
Mapambano yake hata hivyo hayashindanii mataji rasmi japo kwa vyovyote vile, mikeke yake na mashamsham inasaidia kuuza tikiti kwa wingi jambo ambalo linamfaa yeye pia kifedha.
Lakini wataalamu wanaonya asipo tahadhari, huenda akapata jeraha mbaya.