Maandalizi ya timu ya taifa ya kandanda ya Kenya Harambee Stars yanazidi kuimarika huku dalili zote zikiashiria kuwa kikosi hicho kiko tayari kuchuana na Urusi, mechi ya kirafiki iliyoratibiwa kuchezwa jumatatu, Oktoba 16, 2023, mjini Antalya, Uturuki.
Kenya inatarajia ushindani mkali kutoka Warusi huku wawili hao wakikwatuana katika mechi inayotabiriwa kuwa na mvuto mkubwa kwani ni mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu Kenya kuchuana na timu 40 bora duniani huku Urusi ikishikilia nafasi ya 39 kwa viwango vya mataifa bora vya FIFA.
Kocha Firat amesifu mechi ya kirafiki dhidi ya Urusi akitaja kuwa ni mojawapo ya juhudi za Kufungua milango kwa Soka ya Kenya.
"Mechi hizi za kirafiki sio tu ya kuangazia matokeo bali zinatoa fursa kwa soka ya Kenya, " alisema kocha Firat.
"Nina matumaini kwamba mechi hizi, mbali na kuwaweka wachezaji wetu katika nafasi nzuri ya kuwapa fursa, pia zitachangia kuuza soka ya Kenya, na kwa muda mrefu, zitazalisha kipato kwa vilabu vya Kenya kupitia ada za uhamisho," aliongeza kocha huyo.
Mlinzi matata Johnstone Omurwa anayecheza soka ya kulipwa nchini Ureno amejiunga na kikosi hicho 2023 na kumwezesha kocha Engin Firat kukamilisha kikosi chake.
"Tunajihisi tuko tayari na nina matumaini kuwa ifikapo mwezi ujao, tutakuwa tayari kabisa kwa mechi za kufuzu, " alisema Kiungo wa kati Kenneth Muguna.
Harambee Stars imeshirikishwa Kundi F ikiwa kundi moja na Ivory Coast, Gabon, Gambia, Burundi, na Ushelisheli kwa minajili ya mechi za kufuzu Kombe la dunia FIFA 2026 zitakazoanza kupigwa mwezi Novemba mwaka huu.
Walinda lango: Patrick Matasi, Brian Bwire, Bryne Odiambo
Mabeki: Joseph Stanley Okumu, Brian Mandela, Johnstone Omurwa, Collins Sichenje, Erick Ouma, Rooney Onyango, Daniel Sakari, Vincent Harper, Amos Nondi
Viungo wa kati: Richard Odada, Anthony Akumu, Kenneth Muguna, Alpha Onyango, Ayub Timbe, Ovella Ochieng
Washambuliaji: Masoud Juma, Alfred Scriven, Cliffton Miheso, Moses Shummah, Michael Olunga