Timu za soka za wanawake za Tanzania na Kenya zitaanza safari ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa Bora Afrika kwa Wanawake litakalofanyika Morocco mwaka 2024 baada ya mechi za Kufuzu kuanza rasmi siku ya Jumatano.
Timu zote za kina dada kutoka Ukanda wa CECAFA zimeanza safari yao ya kufuzu kwa kupoteza mechi zote huku Rwanda, Uganda na Sudan Kusini zikilazwa mechi za Jumatano.
Kenya imeendelea na mazoezi yake ikijiandaa kupiga mechi yao ya kwanza ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake 2024 (WAFCON) dhidi ya Cameroon leo Ijumaa , huko Douala, Cameroon.
Kwa upande mwingine, Twiga Stars ya Tanzania nayo imezidi kuendelea na mazoezi yake katika uwanja wa shule ya sekondari ya sayansi Yamoussoukro nchini Ivory Coast.
Baada ya kushuka dimbani Ijumaa, timu ya Tanzania itakuwa mwenyeji kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, tarehe 26 Septemba.
Starlets watategemea huduma za mshambuliaji matata Esse Akida ambaye amerudi kwa kikosi cha timu ya taifa kwa mara ya kwanza tangu 2018 baada ya kuchangia pakubwa na kuwa kwenye kikosi kilichoipeleka Kenya kutua WAFCON mwaka huo huo.
Ingawa timu hiyo ina kibarua dhidi ya Cameroon, iwapo itajizolea ushindi katika mechi hizo mbili za kufuzu, itavuka kukabiliana na Gabon au Botswana katika raundi ya pili, iliyoratibiwa kuchezwa kati ya Novemba 27 na Desemba 5, 2023.
Siku ya Jumatano, timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Uganda, Crested Cranes, ilikuwa mwenyeji wa Algeria katika uwanja wa Kituo cha Ufundi cha shirikisho la soka Uganda, FUFA, huku ikifungua safari yake kwa kufungwa 2-1 na Waalgeria katika mechi ya raundi wa kwanza.
Uganda inalenga kurejea Kombe la Afcon kwa wanawake kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kushiriki makala ya mwisho yaliyofanyika Morocco mwaka jana.
Kwenye matokeo mengine, Rwanda ilicharazwa 7-0 na Ghana huku nyota wa Black Stars Evelyn Badu akidhihirisha ni kwa nini alichaguliwa chipukizi bora wa kike wa mwaka katika Tuzo za mwisho za CAF baada ya kufunga mabao mawili na kuitesa Rwanda.
Wakati huo huo, mabinti wa Sudan Kusini walirejea kutoka Misri baada ya kulishwa mabao manne na kuzamisha matumaini yao inapoelekea mechi ya mkondo wa pili.
Mechi zaidi zimepangwa kuchezwa leo huku Burundi ikimenyana na Ethiopia katika Uwanja wa Abebe Bekila, Addis Ababa.