Timu ya Taifa ya Ufaransa imejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali baada ya kuifunga Ubelgiji bao 1-0, katika mchezo wa raundi ya mtoano ya michuano ya UEFA EURO 2024, inayoendelea nchini Ujerumani.
Kiungo mkabaji, N’Golo Kanté alipenyeza pasi safi kwa mshambuliaji wa Paris Saint Germain, Randal Kolo Muani, ambaye bila hiyana, aliachia shuti lililombabatiza beki Jan Vertonghen wa Ubelgiji na kumpeleka marikiti kipa wake Koen Casteels, kisha kutinga wavuni.
Bao hilo la dakika za lala salama, liliwavunja moyo wachezaji wa Ubelgiji, waliokuwa wakiongozwa na nahodha wao, Kevin De Bruyne hasa baada ya kuwa wameonesha kandanda safi katika mchezo huo uliorindima kwenye uwanja wa Dusseldorf Arena, nchini Ujerumani.
Kwa sasa, Ufaransa inasubiri mshindi wa mchezo kati ya Ureno na Slovenia, huku ikijiandaa kujitupa tena uwanjani Julai 5, 2024.