Didier Drogba anawataka wachezaji kuzingatia na kutegemea uchezaji. Picha: AFP

Mshambulizi wa zamani wa Chelsea Didier Drogba anasema wachezaji wa kandanda barani Afrika mara nyingi hutegwa na mawakala feki wanaouza ahadi za umaarufu na utajiri.

Kupitia taasisi yake, Drogba ameungana na chama cha wachezaji wa soka duniani FIFPRO na Shirika la Kazi Duniani ili kuongeza ufahamu kuhusu hatari hizo.

"Tafadhali, nahitaji usikie hili," mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ivory Coast Drogba anasema katika video ya uhuishaji ya kampeni kwa wachezaji. "Kuwa makini sana unayemwamini. Kamwe usimwamini mtu anayetaka pesa zako."

Hivi majuzi FIFPRO ilichunguza wachezaji 263 kutoka nchi saba za Afrika na kugundua kuwa zaidi ya 70% walitafutwa bila wao kuuliza, na mtu ambaye aliahidi kuwasaidia kubadili klabu.

Hatari kwa wachezaji

Mara nyingi, wachezaji waliofikiwa walipewa nafasi ya majaribio (43%) au mkataba na klabu (39%) - na 56% hawakupata majaribio waliyoahidiwa, wakati 44% hawakusaini mkataba ambao walitarajia.

"Ukweli unasikitisha sana... Katika baadhi ya hali mbaya zaidi wachezaji hujikuta wakihangaika nje ya nchi bila pesa za kurejea nyumbani." Wachezaji vijana haswa, Drogba alisema, wako hatarini kwa hamu yao ya kupata wakala.

"Wakala wako bora sio mtu ambaye unaweza kumwamini, wakala bora unayeweza kuwa naye ni uchezaji wako," Drogba alisema kwenye simu ya video wiki hii na wanahabari. "Hii kamwe haidanganyi. Kwa hivyo kadri unavyocheza zaidi, ndivyo vilabu vingi vinakuja kukutazama ukicheza.

"Ninachokiona ni watoto wengi wanaotafuta wakala wa kunitafutia klabu. Hivyo sivyo inavyofanya kazi. Ni utendaji mdio utakao wavutia vilabu na mawakala wazuri."

TRT Afrika