Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya DRC./Picha: Fecofa X

Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ndio timu bora zaidi kwa upande wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa viwango vya ubora wa soka wa mataifa mbalimbali uliotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Juni 20, 2024, DRC inashika nafasi ya 61, ikiwa imepanda juu kwa nafasi mbili, na hivyo kuongoza ukanda wa Afrika Mashariki.

Chui hao kutoka DRC walishika nafasi ya nne katika makala ya 34 ya michuano ya AFCON 2023 yaliyofanyika nchini Ivory Coast.

Ikiwa imedondoka kwa nafasi mbili ulimwenguni, Uganda iko katika nafasi ya 94 na ni ya pili kwa ubora wa Soka katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikifuatiwa na Kenya, ambayo imeporomoka kwa nafasi moja chini na kuwa ya 108 duniani.

Nafasi ya nne kwa ubora wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki inakwenda kwa Tanzania, ambaye imepanda kwa nafasi tano hadi ya 114 duniani. Hivi karibuni, Taifa Stars iliifunga Zambia goli 1-0 katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia kwa mwaka 2026.

Kama ilivyo kwa DRC, 'Taifa Stars' nayo ilishiriki michuano ya AFCON 2023. Hata hivyo, Tanzania ilikuwa ya mwisho kwenye msimamo wa kundi F, baada ya kuambulia alama mbili kwenye mashindano hayo makubwa na yenye hadhi barani Afrika.

Rwanda ni ya tano kwa ubora ikiwa na alama 132, ikifuatiwa na Burundi ambayo ipo katika nafasi ya 140 duniani, wakati Sudan ya Kusini na Somalia zikiambulia nafasi ya 167 na 202 mtawalia.

TRT Afrika