Mauro Icardi aliipa Galatasaray ushindi wake wa kwanza kwenye ardhi ya Uingereza. Picha: UEFA

Matokeo ya kushangaza ni ushindi wa Galatasaray ya Uturuki ambayo imeipiga Manchester United 3-2 ugani Old Trafford, katika kipute cha kuvutia cha timu za kundi A.

Man United 2-3 Galatasaray

Ushindi huo ulikuwa ni wa kwanza wa Galatasaray kwenye ardhi ya Uingereza huku ikiwa pia ni mara ya kwanza kwa United kupoteza mechi mbili za mwanzo za makundi katika ligi ya Mabingwa.

Mshambulizi wa United Rasmus Højlund aliiweka United kifua mbele, kabla ya Wilfried Zaha kusawazisha dhidi ya klabu yake ya zamani. Højlund alirejesha uongozi wa United na goli la pili, lakini Waturuki walisawazisha tena kupitia Kerem Aktürkoğlu.

Mauro Icardi alirekebisha kosa la kutofunga penalti kwa kupachika goli la ushindi dakika chache baadaye.

Copenhagen 1-2 Bayern

Bayen Munich imeponea kichapo baada ya magoli ya Jamal Musiala na Mathys Tel kuisaidia Bayern kutoka nyuma jijini Copenhagen baada ya wenyeji kuchukua uongozi kupitia Lukas Lerager.

PSV Eindhoven 2-2 Sevilla

Sevilla ya Uhispania ilijipatia uongozi licha ya kuwa ugenini kupitia beki Nemanja Gudelj kabla ya nahodha wa PSV Luuk De Jong kusawazisha kupitia penalti.

Aidha, ilionekana kuwa mshambuliaji wa Sevilla Youssef En Nesyri aliwapa wageni ushindi kupitia kichwa kabla ya Jordan Teze kuwasawazishia wenyeji PSV.

Lens 2-1 Arsenal

Ingawa Arsenal waliongoza mapema kupitia Gabriel Jesus, wenyeji Lens walitoka nyuma na kuwalaza the Gunners 2-1 kupitia mabao ya Adrien Thomasson na Elye Wahi.

Arsenal ilifaya juhudi zote ikitafuta bao la kusawazisha, lakini ulinzi wa Lens ulionekana kuwa wenye nguvu na uliopangwa vizuri.

Napoli 2-3 Real Madrid

Real Madrid ilitoka nyuma kuimaliza Napoli Katika ngoma ya kusisimua ya mabao matano huko Naples na kuchukua uongozi wa kundi C.

Napoli ilitangulia kupitia Leo Østigård lakini Vinícius júnior aliisawazishia Madrid kabla ya Jude Bellingham kuponyoka kutoka katikati na kutundika shuti wavuni. Hata hivyo, baadaye Piotr Zieliński aliirejesha Napoli mechini kabla ya mkwaju wa Federico Valverde kumduwaza mlinda lango Alex Meret na kuizolea Real Madrid ushindi zikiwa zimesalia dakika 12 kabla ya mechi kukamilika.

Kwenye matokeo mengine, Salzburg ilipoteza 0-2 dhidi ya Real Sociedad huku Inter ikijipa ushindi wa 1-0 dhidi ya Benfica.

TRT Afrika