Tanzania na Zanzibar zinazidi kutamalaki soka ya wanasoka chipukizi ukanda wa Afrika Mashariki baada ya timu hizo mbili za vijana wasiopungua miaka 18, kujinyakulia ushindi wa 1-0 dhidi ya majirani Uganda na Sudan Kusini mtawalia.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Zanzibar kuipiga Uganda 4-3 kwenye penalti mechi ya fainali na kushinda kombe la kikanda la Cecafa U15 2023, lililoandaliwa Uganda.
Ushindi wa leo umeiwezesha Tanzania kufungua safari yake ya mashindano ya Cecafa U-18 kwa wavulana 2023, yaliyoanza nchini Kenya Jumamosi, kwa furaha.
Goli la kipekee katika mechi hiyo lilipachikwa wavuni na nyota Sharif Wilson kupitia frikiki kunako dakika ya 31.
Wakati huo huo, Zanzibar U-18 nao wameanza safari yao ya CECAFA U-18 kwa ushindi kwani bao la Mohamed Ali katika dakika ya 13 lilitosha kuipa ushindi wa 1-0 dhidi ya Sudan Kusini.
Mnamo Jumamosi, Harambee Stars ya Kenya ilijinyakulia ushindi wa 5-0 ikijipa motisha kwa kucheza mbele ya mashabiki wao wa nyumbani na kuiadhibu Sudan ngarambe ya Kundi A iliyogaragazwa katika Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu.
Kwenye mchuano mwingine ulioshuhudiwa Jumamosi, Rwanda iliilaza Somalia 1-0 baada ya Sibomana Sultan Bobo kumduwaza kipa wa Somalia Mohamed Abdikadir.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Djibouti (FDF) liliondoa timu yao kutoka kombe hilo la Wavulana la Cecafa U-18 licha ya kualikwa.
Kundi A: Kenya, Somalia, Rwanda, Sudan
Kundi B : Tanzania, Zanzibar, Sudan Kusini, Uganda