CAF hapo awali ilikubali kushindwa kumudu kalenda ya michuano ya kimataifa inayoonekana kugongana.   / Picha : CAF 

Fainali zinazotarajiwa za Kombe la Mataifa ya Afrika zimesogezwa mbele kwa miezi sita na sasa zitachezwa kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lilitangaza Ijumaa.

CAF pia imeahirisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake kwa mwaka mzima hadi Julai 5-2026. Hiyo pia inaandaliwa nchini Morocco.

Tarehe za michuano hiyo miwili zimekuwa zikitazamiwa kwa hamu kwani CAF hapo awali ilikubali kushindwa kumudu kalenda ya michuano ya kimataifa inayoonekana kugongana.

"Kutangazwa kwa tarehe za AFCON nchini Morocco 2025 kulichukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa, kwani kulikuwa na mijadala migumu na wakati fulani yenye changamoto na wahusika mbalimbali, kwa kuzingatia kalenda ya mechi za kimataifa na za ndani," alisema rais wa CAF Patrice Motsepe.

Motsepe pia alisisitiza kuwa maandalizi yatakuwa ya hali ya juu zaidi ya michuano hiyo.

"Nina imani kuwa CAF TotalEnergies AFCON Morocco 2025 itakuwa ya mafanikio makubwa na itakuwa AFCON bora zaidi katika historia ya mashindano haya,'' aliendelea kusema.

Migongano ya mechi za Afrika na Ulaya

Katika taarifa yake, Motsepe pia alipongeza ukuaji mkubwa uliodhihirika katika soka ya wanawake barani Afrika akisema shirikisho hilo litajitolea kwa vyovyote kukuza vipaji vywa wasichana kufikia ushindani mkali wa kimataifa.

CAF imekuwa ikisutwa na changamoto ya kuainisha tarehe za mashindano yake barani Afrika kuepusha migongano na mivutano na michuano mengine kimataifa hasa kutokana na kuwa wachezaji wengi wa timu na vilabu vya mataifa yao, ni wachezaji mahiri wanaotegemewa pia katika vilabu Ulaya na kwengineko.

Mara nyingi makocha wa Ulaya wamekuwa wakilalamika wanapolazimika kuwaachilia wachezaji wao kwenda kuwakilisha timu zao za taifa katika michuano ya bara na hivyo kukosa kuorodheshwa katika vikosi vya klabu.

''CAF imejitolea kulinda na kuendeleza maslahi ya wachezaji wa Kiafrika, wanaocheza katika vilabu vya soka barani Ulaya na duniani kote,'' alisema Motsepe katika taairfa yake. ''CAF pia imejitolea kujenga uhusiano wenye manufaa kwa ECA, UEFA, Mashirikisho mengine ya Soka na FIFA,'' aliongeza kusema.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya mkutano wa baraza kuu la usimamizi la CAF uliofanyika Ijumaa kwa njia ya video.

Mkutano huo pia ulitangaza kufunguliwa zabuni ya nani atakayeandaa michuano kadhaa ijayo ikiwemo Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya CAF 2024, CAF TotalEnergies U17 AFCON, CAF TotalEnergies U20 AFCON na Tuzo za CAF 2024.

TRT Afrika na mashirika ya habari