CAF imeanzisha uchunguzi dhidi ya Shirikisho la Soka la flame ya kiarabu ya Morocco (“FRMF”) na Shirikisho la Soka la Congo (“FECOFA”) kufuatia matukio ya baada ya mechi wakati wa mechi ya TotalEnergies CAF Kombe la Mataifa ya Afrika Cote d'Ivoire 2023 kati ya Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika taarifa fupi kwenye tovuti yake, CAF ilisema kuwa uchunguzi huo umeanza na kuongeza kuwa haitazungumzia suala hili tena hadi uchunguzi utakapo kamilika.
Nini chanzo cha ugomvi kati ya Morocco na DRC katika mechi yao ?
Katika mechi ya kusisimua sana Jumapili, Morocco ilitoka sare ya 1-1 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Kundi F.
Beki wa kulia, na nyota wa Morocco, Achraf Hakimi aliifungia timu yake bao la mapema dakika ya sita kwenye Uwanja wa Laurent Pokou mjini San Pedro, Ivory Coast.
Mshambulizi wa DR Congo, Silas Katompa Mvumpa alisawazisha bao hilo dakika ya 76.
Hata hivyo mzozo ulionekana kuzuka kati ya wachezaji wa pande hizo mbili na wakufunzi baada ya kocha wa Morocco Walid Regragui kumwendea nahodha wa Congo, Chancel Mbemba, ambaye alipokea kadi ya njano kwa kugombana na mwamuzi.
Kwa mtazamo wa picha uwanjani:
- Regragui alimtafuta Mbemba baada ya mechi huku mchezaji huyo akiwa amepiga magoti.
- Mbemba alichukua mkono wa Regragui na kumpigapiga mgongoni, akionekana kudhani ni mazungumzo ya kirafiki.
- Lakini Regragui alishika mkono wa Mbemba kuuzuia na kuendelea kuongea.
- Mchezaji huyo alitoa mkono wake kwa hasira na kumuashiria mwamuzi wa video kabla ya wachezaji wa pande zote mbili kuingilia kati.
- Punde wachezaji kutoka pande zote mbili walionekana kuelekea katika tukio huku wenigne wakiwa na ghadhabu. Licha ya kuondoka uwanjani mzozo unasemekana kuendelea hadi eneo la kuelekea vyumba vya wachezaji.
Mbemba alinukuliwa baada ya mechi huko San Pedro kusema kuwa Regragui alikuwa amemtusi.
"Ninakaa kimya, ni bora zaidi. Kila mtu ananifahamu, naheshimu kila mtu. Lakini sikuwahi kufikiria kuwa ningesikia maneno haya kutoka kinywani mwa kocha," Mbemba alisema.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa Regragui.
Tangu zogo hilo kutokea siku ya Jumapili, nahodha wa DRC Chancel Mbemba alikumbwa na wimbi la unyanyasaji wa kibaguzi kwenye mitandao ya kijamii.
Akaunti yake ya Instagram ililengwa na watumiaji wengi ambao walijibu machapisho yake ya hivi punde kwa kutumia emoji za tumbili au sokwe, au waliandika maoni ya ubaguzi wa rangi.
Japo haijabainika ubishi kati ya kocha wa Morocco, Regragui na Mbemba ulikuwa juu ya nini, kumekuwa na madai kuwa ulihusu ubaguzi wa rangi, jambo ambalo halijathibitishwa hadi sasa.
Shutuma kama hizi za ubaguzi wa rangi ziliibuka pia wakati wa kombe la dunia ambapo Morocco, timu ya pekee ya Afrika kufika nusu fainali, ilijisifia kama nchi ya kiarabu na kusababisha shutuma kali kutoka kwa mashabiki wa Kiafrika.
Timu ya Morocco pamoja na mashabiki wao wamekanusha madai yoyote ya ubaguzi wa rangi.