Timu ya Burnley sasa itashiriki michuano ya 'Championship', baada ya kufungwa mabao 2-1, na Tottenham Hotspur Mei 11, 2024, na hivyo kushuka kutoka daraja la Ligi Kuu ya Uingereza.
Burnely, inayonolewa na mlinzi wa zamani wa Manchester City, Vincent Kompany ikiwa nafasi ya 19, baada ya kukusanya alama 25 tu, ndani ya michezo 37, na hivyo kuondoa kabisa matumaini yao ya kusalia kwenye Ligi hiyo.
"Tutakuwa kwenye mashindano ya 'Championship' msimu ujao. Mwisho wa hadithi nzuri. Ahsanteni kwa kutuunga mkono," lilisomeka chapisho kwenye ukurasa rasmi wa X wa klabu hiyo kutoka Lancashire.
Katika mchezo huo, Burnley ndio walikuwa wa kwanza kupata bao, kupitia kwa Jacob Bruun Larsen, katika dakika 25.
Pedro Porro aliisawazishia Tottenham Hotspur dakika chache baadae baada ya kuachia shuti kali, nje kidogo ya eneo la hatari.
Mchezaji wa kimataifa kutoka Uholanzi, Micky van de Ven akaongeza la pili kwa Tottenham katika dakika ya 82 ya mchezo, na hivyo kuwashusha rasmi vijana wa Kompany kutoka Ligi Kuu ya Uingereza.