Bukayo Saka wa Arsenal akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la pili dhidi ya Wolves kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya EPL uliofanyika Agosti 17, 2024 kwenye Uwanja wa Emirates./Picha: Getty

Klabu ya Arsenal ya Uingereza imeuanza vyema msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza maarufu kama EPL baada kuifunga Wolverhampton Wanderers, mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Emirates.

Mabao ya The Gunners yalitiwa kimiani na Kai Havertz na Bukayo Saka na kuwapa vijana wa Mikel Arteta alama 3 muhimu katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi hiyo maarufu duniani.

Havertz aliifungia Arsenal bao la kuongoza kwa njia ya kichwa kufuatia krosi tamu ya Saka katika dakika ya 25 ya mchezo.

Licha ya kutanguliwa kufungwa, Wolves walionekana kuimarika kimchezo, wakiongeza mashambulizi dhidi ya vijana wa Arteta.

Wolves walitengeneza nafasi za kuzawazisha bao hilo kupitia kwa Rayan Ait-Nouri na Rodrigo Gomes, lakini mlinda lango wa 'Washika bunduki wa jijini London', David Raya alikuwa imara, katika mchezo ambao Saka aling'ara.

TRT Afrika