Beki wa kimataifa wa Kenya Joseph Okumu amesajiliwa na Stade de Reims inayocheza kwenye Ligi ya Ufaransa 'Ligue 1' kwa kusaini mkataba wa miaka 5 huku akikabidhiwa jezi nambari mbili.
Stade de Reims iliyomaliza katika nafasi ya kumi na moja kwenye jedwali la ligi hiyo msimu uliopita, imetangaza kumnasa kiungo huyo kwa kitita cha Euro milioni 12 kutoka KAA Gent ya Ubejgiji.
Okumu, mwenye umri wa miaka 26, aliiaga klabu yake ya Gent ya Ubelgiji kwa kuiachia ujumbe kwenye kurasa zake mitandano.
"Wapendwa Buffalos, miaka miwili nanyi imekuwa ya kukumbukwa. Safari yangu na muda wangu nanyi umekuwa mzuri. Wachezaji, wafanyakazi na mashabiki wamekuwa wa kushangaza. Asante Gent kwa kumbukumbu. Proost!!"
Mkurugenzi Mtendaji wa KAA Gent Michel Louwagie, amemtakia Okumu kila la heri huku akimsifia kwa kuitumikia klabu hiyo kikamilifu baada ya kuiwakilisha kwa mechi 92 alipojiunga nao kutoka Elfsborg mnamo 2021.
“Okumu ametoa huduma bora kwa klabu yetu. Pamoja na mabeki Ngadeu na Torunarigha, aliunda ukuta mkali sana kwenye ulinzi. Joseph alijisikia tayari kuchukua hatua inayofuata katika kazi yake na amefurahia uhamisho wake Reims. Sasa ni juu yetu kujaza nafasi aliyoacha kwa njia nzuri. KAA Gent inamtakia mafanikio mema katika klabu yake mpya nchini Ufaransa. Kila la heri Joe!"
Mnamo mwaka wa 2014, mlinzi huyo alipata umaarufu akiwa mchezaji chipukizi wa tiku ya soka ya shule ya sekondari ya Kakamega iliyotwaa ubingwa wa mashindano ya kitaifa ya soka kwa kuishinda Kisumu Day.
Kabla ya kusajiliwa na Reims, safari ya Okumu kwenye soka ya kulipwa ilmwezesha kucheza katika vilabu vya Chemilil Sugar nchini Kenya, Free State ya Afrika Kusini, AFC Ann Arbor na Real Monarchs ya Marekani, IF Elfsborg ya Uswidi, na KAA Gent ya Ubejgiji.