Arsenal waliweka ulinzi mkali, wakiondoa hatari zote za mabingwa wa Ligi kuu hadi John Stones aliposawazisha / Picha: Reuters

Arsenal ililazimika kucheza ikiwa na wachezaji 10 baada ya Leandro Trossard kulishwa kadi ya pili ya njano kwa kupiga mpira mbali Arsenal ikiongoza 2-1 mwishoni mwa kipindi cha kwanza uwanjani Etihad, Jumapili.

Baada ya mapumziko 'Gunners' waliketi nyuma na kuweka ngome kali, wakitoa karibu hatari zote za mabingwa wa Ligi kuu hadi John Stones alipofunga bao la kusawazisha sekunde za mwisho.

Arsenal, ambao walikuwa wameongoza kwa sehemu kubwa ya pambano hilo, baada ya mabao kutoka kwa Riccardo Calafiori na Gabriel Magalhaes, walilaumiwa kwa kutumia "mbinu zisizofaa" na mabeki wa Man City, Kyle Walker na Stones.

Mshambuliaji wa City Bernardo Silva aliwashtumu pia kwa "kupoteza muda".

Hata hivyo, kocha wa Arsenal Arteta alisimama na mbinu ya timu yake, akirejelea kupoteza 5-0 dhidi ya Manchester City mnamo 2021, wakati nahodha wake wa zamani Granit Xhaka alipolishwa kadi nyekundi na kuondoka uwanjani.

Akizungumza kuelekea mechi ya Jumatano ya raundi ya tatu ya Kombe la ligi dhidi ya Bolton ya daraja la tatu, Mhispania huyo alisema timu yake "ililazimika kucheza mchezo namna ambayo ilicheza".

"Kwa bahati mbaya tumekuwa katika hali hiyo hiyo awali," alisema. "Tulikuwa katika hali hiyo hiyo na Granit na wakati tulipopoteza 5-0. Kwa hivyo ni bora tujifunze. Ikiwa sivyo ningekuwa mjinga sana."

Erling Haaland alitupa mpira kwenye kichwa cha mlinzi wa Arsenal Gabriel baada ya City kusawazisha wakati hasira zilipokuwa zikipanda lakini Arteta alipuuza mvutano huo.

"Tayari tunaganga yajayo na sasa tuko tayari kupigana tena kesho," alisema.

Aliongeza, "Timu, hamu ambayo wanapaswa kushindana katika muktadha wowote, kushinda, kuzoea hali tofauti, mashindano tofauti, njia tofauti za kucheza na kushughulikia hilo kisaikolojia na kimwili, njia ambayo tumefanya ni nzuri sana."

Arteta aliongeza kwa utani kwamba angewaambia wachezaji wake waachane na mpira kuelekea mechi zijazo baada ya kadi ya pili ya njano ya Trossard.

Awali, Declan Rice pia alionyeshwa njano ya pili kwa kupiga mpira mbali katika sare ya Arsenal dhidi ya Brighton mwezi uliopita.

"Acha tu mpira, usiguse mpira," alisema. "Tutacheza bila mpira."

Arteta alitoa taarifa kuhusu nahodha aliyejeruhiwa Martin Odegaard, akisema kurejea kwake kutoka kwa jereha lake la mguu ni "suala la wiki kadhaa".

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 amekosa michezo mitatu iliyopita ya Gunners baada ya kuumia katika mechi ya kimataifa akiwakilisha Norway mapema mwezi huu.

"Nadhani ni suala la wiki kadhaa, lakini siwezi kueleza itakuwa kwa muda gani," alisema.

AFP