Klabu ya Arsenal ya Uingereza imepata ushindi dhidi ya Manchester City katika mechi ya ligi kuu ya Soka nchini Uingereza iliyogaragazwa uwanjani Emirates.
Kabla ya mechi ya Jumapili, Arsenal haijawahi kuipiga Manchester City katika ligi hiyo tangu Disemba 2015, mwaka mmoja kabla ya Pep Guardiola kuchukua nafasi hiyo.
Wakati huo huo, Arsenal walipoteza mechi zao 12 za mwisho za Ligi kuu dhidi ya City, wakifanikiwa tu kufunga mabao matano tu na kuzabwa jumla ya mabao 33 katika kipindi hicho.
Goli la Gabriel Martinelli dakika ya 86 limeiwezesha Arsenal kukata minyororo ya kutawaliwa na City kwani kabla ya mechi ya leo, rekodi yake na City ndio msururu wa matokeo duni dhidi ya mpinzani katika historia ya Arsenal kwenye ligi.
Pasi ndefu kutoka kulia ilimpata beki Tomiyasu kwenye sanduku, kabla ya kumwahi Mjerumani Havertz, aliyemuandalia Mbrazili, Martinelli.
Martinelli ambaye alichukua nafasi ya Trossard katika mabadiliko yaliyofanywa na Arteta dakika ya 46, aliachilia kombora lililomwahi Ake na kumduwaza Ederson.
Baada ya ushindi huo ulioipa Arsenal alama tatu muhimu, Arsenal imejiunga na Tottenham Hotspur kileleni mwa ligi wakiwa na pointi sawa lakini tofauti tu kwa idadi ya mabao.
Mbinu za Arteta za kuwaondoa Zinchenko, Nketiah na Jorginho na kuwachezesha Havertz, Partey na Tomiyasu zilionekana kufua dafu huku ulinzi wa Arsenal ukifanya juhudi na kusajili ushindi huo wa kihistoria.
Kwa kocha Arteta, ushindi dhidi ya City umekuwa na umuhimu mkubwa kwani, licha ya kuzipiga timu 23 kati ya 24 alizokabiliana nazo kama meneja katika ligi kuu, alishindwa tu kuinyuka Man City, huku akipoteza mechi yake yote saba dhidi ya Manchester City.
Aidha, Arsenal haijawahi kumaliza mechi bila kufungwa bao na Man City kila walipokutana ikiwemo mechi zao 16 za mwisho za ligi kuu dhidi ya Man City, tangu ushindi wao wa 2-0 ugenini mnamo Januari 2015.
Kwa sasa Arsenal inajiandaa kuchuana na Chelsea ugenini Jumamosi terehe 21 October 2023 huku ligi hiyo ikiingia mapumziko kwa ajili ya mechi za kimataifa.
Matokeo ya mechi za Jumapili tarehe 8 Oktoba 2023
- Brighton 2-2 Liverpool
- West Ham 2-2 Newcastle
- Wolves 1-1 Aston Villa
Matokeo ya mechi za Jumamosi tarehe 7 Oktoba 2023
- Luton 0-1 Spurs
- Burnley 1-4 Chelsea
- Everton 3-0 Bournemouth
- Fulham 3-1 Sheffield Utd
- Man Utd 2-1 Brentford
- Crystal Palace 0-0 Nottingham Forest