Arda Güler ndiye mchezaji wa kwanza kutoka Uturuki kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kiungo huyo mshambuliaji mwenye miaka 19 anaingia kwenye vitabu vya historia baada ya timu yake ya Real Madrid kutoka hispania kuifunga Borussia Dortmund ya Ujerumani mabao 2-0, katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa Juni 1, 2024 kwenye uwanja wa Wembley nchini Uingereza.
Julai 6, 2023, Real Madrid ilitangaza kumsajili nyota huyo wa timu ya taifa ya Uturuki kwa mkataba wa miaka sita, hadi Juni 2029.
Waturuki wengine ambao wamewahi kuichezea klabu ya Real Madrid kabla ya Arda Güler ni pamoja na Hamit Altintop na Nuri Şahin
Mlinzi wa hispania Dani Carvajal na mshambuliaji kutoka Brazil Vinicius Jr waliwafungia mabingwa hao wa La Liga mabao katika dakika ya 74 na 83 ya mchezo, na kuiwezesha Real Madrid kutwaa taji hilo kwa mara ya 15.
Taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya linakuwa la sita ndani ya miaka 10 kwa Real Madrid, klabu iliyoanzishwa mwaka 1902.