Na Charles Mgbolu
Tasnia ya burudani nchini Nigeria imelaani vikali dhihaka na kejeli za mitandaoni dhidi ya mchezaji Alex Iwobi, baada ya Super Eagles kushindwa kubeba kombe la AFCON 2023, mbele ya wenyeji Côte d'Ivoire.
Muimbaji Falz, mchekeshaji AY Makun pamoja na mtangazaji wa radio Dotun ni baadhi tu ya watu waliotumia kurasa za mitandao yao ya kijamii kumkingia kifua Iwobi kufuatia kiwango alichokionesha kwenye michuano hiyo.
"Kila mchezaji anayevaa jezi ya kijani na nyeupe kuiwakilisha Nigeria amejitoa sadaka kubwa sana, haipendezi kuona wakifanyiwa dharau ya namna hiyo.
Tunazungumza sana kuhusu unyanyasaji mitandaoni, lakini ni rahisi sisi wenyewe kugeukana. @alexanderiwobi nakupenda ndugu yangu! Ahsante," aliandika Falz kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Falz aliambatanisha hisia zake na picha ya nyota huyo yenye maneno "Tunashinda pamoja, tunapoteza pamoja. Katika ukurasa wake, AY Makun, alilaani manyanyaso mitandaoni na kuwaasa mashabiki kuwa na utamaduni wa kuonesha kujaliana.
"Inasikitisha kuona namna tulivyotumia majukwaa yetu tofauti dhidi ya kijana huyu kwa kosa tu la kuiwakilisha nchi ya baba yake. Kesho, mtatambua sababu kwa nini wachezaji kama Saka na wengine hawatochezea Nigeria kamwe.
''Ni wakati muafaka kuangalia nje ya maslahi yetu binafsi na kuangazia madhara hasi ya matendo yetu. Tukuze utamaduni wa upendo, kujaliana na heshima kwenye mitandao na tuzuie aina zote za manyanyaso kwenye majukwaa hayo.
Tumuonyeshe @alexanderiwobi kwenye andiko hili,” alisema Makun. Mtangazaji wa redio, Dotun alitumia mtandao wake sio kwa kulaani manyanyaso mitandaoni, lakini alitumia fursa hiyo kumuomba Iwobi msamaha.
‘’Naweza nikawa nimeumizwa kwa kupoteza mchezo ule. Ndio, lakini sijakasirika kwa sababu timu yetu ilijitahidi kadiri ya uwezo wake. @alexiwobi kushambuliwa sio kitu kizuri, nadhani tunahitaji kukubali kufungwa bila kuwaumiza wengine.
Tunaomba msamaha kama tulikufanya ujisikie vibaya,” aliandika Dotun. Iwobi aliamua kutoka kwenye mitandao hiyo, saa chache baada ya kumalizika kwa mchezo huo na pia kuamua kufuta baadhi ya maandiko yake, isipokuwa moja kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Kama ilivyo kwa mashabiki wengi, baadhi ya wachezaji wenzake wameendelea kumpa moyo kufuatia kadhia hiyo. ‘’Tutaondoa hii chuki yote. Tutageuza kejeli na manyanyaso haya kuwa upendo kwa Iwobi,’’ aliandika shabiki mmoja kwenye ukurasa wa X.