Ilikuwa nusu ya kwanza tasa kabisa japo ya kusisimua walipokutana Banyana Banyana wa Afrika Kusini na Usiwidi katika mji mkuu wa New Zealand.
Mshambuliaji Hilda Magaia aliwapatia Waafrika matumaini alipopenyeza kimyani bao la kwanza la mechi dakika tatu tu baada ya kurejea kutoka mapumzikoni.
Thembi Kgatlana alipenyeza ukuta wa Waswidi na kujaribu bahati yake kwa mkwaju mufti japo kipa wa Sweden alikuwa macho naye na kuweza kuusukumia kando. Bahati mbaya kwake mpira ulimuangukia mshambuliaji wa kati Magaia aliyemalizia pigo hilo.
Hata hivyo Afrika Kusini walilipa gharama kubwa kwa bao hilo kwani Magaia alilazimika kuondoka uwanjani punde tu baadaye kutokana na jeraha alilopata.
Sweden wakaona upenyo hapo na wakasawazisha dakika chache baadaye kupitia chenga chenga ya Johana Kaleryd aliayomgusa tu kwa pembeni beki wa Banyana Lebohang Ramalepe na kumfikia Fridolina Rolfo wa Uswidi aliyetikisa wavu dakika ya 65.
Ilikuwa nipe nikupe baada ya hapo na timu zote zilionekana tayari kukubali sare kabla ya dakika ya 90 Uswidi kushangaza uwanja kwa bao la lala salama lililowapa ushindi dhidi ya vigogo hao wa Afrika.
Katika mtandao wao wa Twitter, Banyana walielezea kuwa matokeo yanaumiza roho ila wanakubali na kutazama mbele mechi zijao.
Banyana Banyana sasa wamewekeana miadi na wenzao wa Kundi G Argentina Ijumaa 28.