Waziri Ndumbaro amesema kuwa ziara yake ya Abidjan pia ilikuwa ya  kubalishana mawazo na wenyeji wa mashindano kwa ujumla kuelekea katika maandalizi ya Afcon 2027. / Picha : TRT Afrika

Waziri wa Sanaa, Michezo na Utamaduni wa Tanzania, Damas Ndumbaro amesema kuwa serikali itasalia kuwa nyuma ya timu ya taifa ya Taifa Stars na kudumisha motisha kupitia uboreshaji endelevu wa kiwango cha timu hiyo.

Akizungumza na TRT Afrika, Waziri Ndumbaro amesema kuwa ziara yake ya Cote d'ivoire ni kuipiga jeki timu hiyo kupitia amri ya rais kuhakikisha kuwa timu hiyo inapokea uungwaji tosha kutoka kwa serikali hususan kupitia wizara husika ya michezo.

“Ni muhimu timu zetu ziwe na ubora wa kutosha na hamasa tutakapokuwa wenyeji 2027 na ndio wajibu wetu kufanikisha hilo,” alisema Waziri.

Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa mbali na kuwa na kikosi hicho, pia amekuwa kwenye ziara ya kubalishana mawazo na wenyeji wa mashindano kwa ujumla kuelekea 2027.

“Kutokana na kuwa waandalizi ifikapo 2027, madhumuni ya uwepo wangu hapa ni kujifunza kuhusu maandalizi, miundo mbinu, jinsi ya kuandaa tukio lenyewe, mapokezi, hoteli, mashabiki, uwanjani, na mfumo wa tiketi.”

“Serikali chini ya uongozi wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikitoa motisha kubwa sana kwa timu hii ya taifa stars kwa namna mbalimbali ikiwemo marupurupu, posho na kuhakikisha maandalizi ya timu ni bora zaidi, ndio maana niko hapa,'' aliongeza kusema.

“Nia yetu ni kukuza soka letu ili kuhakikisha kuwa ifikapo 2027, kama waandalizi, tunamaliza kibarua mapema mechini dakika 90 na kujiepusha na hesabu za vidole.”

Safari imekuwa yenye ufanisi na mbali na juhudi na motisha kwa timu, kwa jumla imekuwa ni ziara yenye ufanisi.

Waziri huyo amemaliza kwa kusifu ukuaji wa michezo nchini Tanzania hususan soka kwani matokeo bora ya vilabu vya nchi hiyo vikiwemo vya wanawake kwenye mashindano ya kikanda na bara Afrika, yameizolea Tanzania sifa.

Aidha, amefafanua kuwa ligi kuu ya soka Tanzania bara NBC ni mojawapo ya ligi za bara la Afrika zilizokuwa na uwakilishi mkubwa wa wachezaji kwenye kombe linaloendelea la Afcon.

TRT Afrika