Viongozi wa Afrika wakiwemo marais, Mawaziri Wakuu na viongozi wa serikali wamekutana ili kujadili jinsi nchi za Kiafrika zinazozalisha kahawa zinavyoweza kutumia fursa katika uongezaji thamani na kuongeza mchango wa Afrika katika biashara ya kahawa duniani, yenye thamani inayokadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 466.
Zao la Kahawa ni muhimu kwa uchumi wa Afrika na ni chanzo cha riziki kwa angalau watu milioni 60 katika bara zima.
Mkutano huo wa viongozi wa Afrika unaofanyika Kampala, Uganda ni kongamano la pili la kahawa barani linaloandaliwa na Shirika la Kahawa baina ya Afrika (IACO) kufuatia ufanisi wa mkutano wa kwanza wa G-25 wa Kahawa wa Afrika uliofanyika mjini Nairobi, mnamo mwezi Mei 2022.
Mbali na Wakuu wa Nchi, Mawaziri Waandamizi wa Serikali, miongoni mwa washiriki wengine ni Wakuu wa Mamlaka za Kahawa, Wauzaji kahawa nje ya nchi, Wachoma Kahawa, Vyama vya Kahawa, Wakulima wa Kahawa, na Wasindikaji wa Kahawa.
Ingawa Uganda ni mzalishaji wa pili baada ya Ethiopia, pia ni msafirishaji wa nje zaidi wa kahawa huku ikisafirisha takriban mifuko milioni 6 kwa mwaka zenye thamani ya takriban dola milioni 850.
Miongoni mwa wakuu wa nchi wanaoshiriki kongamano hilo ni Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia Sahle-Work Zewde, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Isdor Mpango, na Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri wa Kenya, Musalia Mudavadi.
Rais wa Equatorial Guinea Teodoro Obiang Nguema Mbasogo na mawaziri wengine wakuu kutoka mataifa 22 yanayozalisha kahawa wanatarajiwa kushiriki mkutano huo.
Mkutano huo wa kilele wa siku tatu utaongozwa na nwenyeji wa mkutano huo, Rais Yoweri Kaguta Museveni na kufikia kileleni siku ya Alhamisi wiki hii.