Mama akimbeba mwanae kwa mapenzi. Picha : Twitter UNICEF

‘’Siku ya Mothers’ Day huwa nampeleka mama yangu kukandwa mwili, namnunulia zawadi ya shada la maua. Kisha namchukua kutengenezwa kucha zake, halafu jioni tunakwenda sehemu kula tukipiga soga.’’

Maneno hayo matamu kutoka kwa Vanya Wanjiru, dada kutoka Kenya akizungumzia njia yake ya kumfurahisha mama yake wakati wa maadhimisho ya siku ya mama duniani.

Maadhimisho haya yanafanyika sehemu mbali mbali duniani tena kwa njia tofauti kabisa.

Mtoto akiandika ujumbe wa siku ya mama duniani. Picha : Reuters

Siku hii watoto huwatolea zawadi mama zao, kama kuonesha shukrani kwa malezi mazuri na mapenzi yasiyokuwa na kifani.

Mwaka huu Mei 14 imetengwa kwa ajili hiyo ambapo kila sehemu utakutana na watu wakinunua maua na zawadi zingine mbali mbali.

Ssangalyambogo Gloria wa Uganda anasema kuwa kama ilivyo ada, amemuandalia mama yake mambo kem kem ya Mothers Day.

Gloria Ssangalyambogo akiwatakia kina mama wote duniani siku kuu njema/ Picha : Gloria Ssangalyambogo

‘’Mimi na ndugu zangu tumeandaa mambo spesheli, natumai atafurahia.’’ Ameongeza, ‘’Namtakia mama yangu na mama wote duniani siku njema ya Mothers day. Mungu awabariki kwa kila mnachowafanyia watoto wenu, tunawapenda sana.’’

Historia: Siku ya Mama Duniani

Siku ya Mama Duniani wakati mwingine inatofautiana kwa tarehe yake. Mwaka huu wengi wanaadhimisha Jumapili mei 14.

Hafla hii inatokana na kumbukumbu za Ugiriki na Roma, ambao wanasemekana walifanya sherehe ya kuwaenzi miungu yao ya uzazi, Rhea na Cybele.

Kuna baadhi wanao shirikisha siku hii na tambiko la wakristu wa zamani, ijulikanayo kama ‘Mothering Sunday.’

Hafla hiyo ambayo ilikuwa maarufu sana katika nchi za Ulaya, na Uingereza, iliadhimishwa Jumapili ya mwisho katika kipindi cha Kwaresma, na ilitazamiwa kama siku ambayo waumini wanarudi nyumbani kuhudhuria misa katika kanisa kuu la eneo lao.

Baada ya muda siku hii ilichukua sura ya kidunia ambapo watoto wanatoa shukran kwa wazazi na walezi wao.

Mama akimbeba mwanae kwa mapenzi. Picha :  UNICEF

Mama ni nani

Kawaida, mama anakuwa yule aliyemzaa mtoto, lakini kutokana na hali ilivyo duniani, baadhi wameanza kuwapa 'hadhi ya mama' walio wafaa kimaisha na malezi hata kama sio mzazi wake.

Baadhi ya waume pia huadhimisha siku hii kwa kuwapa wake zao au mama za wanao zawadi na kuwapongeza kwa malezi bora.

Baadhi ya viongozi wa dunia wametuma ujumbe wao wa pongezi kwa kina mama, katika maadhimisho haya akiwemo mke wa Rais wa Kenya Rachael Ruto.

Anne Kansiime, Msanii na mchekeshaji kutoka Uganda maeandika katika mtandao wake wa Facebook, huku akiwa amempakata mwanae, kuwa,’’ Hakuna kizuri kuliko bahati ya kuwa mama.’’ Ujumbe wake kuonesha raha ya kuwa mama.

Tetesi juu ya siku ya mama duniani

Kumekuwepo baadhi ya tetesi kuwa siku hii wengi wamegeuza kuwa ya kibiashara.

Yaani watu wanafikiria zaidi kuwanunulia mama zao zawadi au kuwatumia pesa na kukosa ile hisia muhimu zaidi ya kuonesha mapenzi kwa mama.

Mmarekani Anna Jarvis, ambaye alisaidia siku hii kusajiliwa Marekani kama siku rasmi ya mama duniani, aligeuka na kuanza kuipinga akisema kuwa imepoteza hadhi yake.

Baadhi ya kina mama waliozungumza na TRT Afrika wametueleza kuwa wanakubali kuwa siku hii ni muhimu kuwa pamoja na wanao kuliko kupokea zawadi tu.

Maua wanazopokea kina mama siku ya maadhimisho ya mothers day. Picha : TRT Afrika

Kwa upande wake Gabriel Lare, mwanamuziki wa Afrika Mashariki anayefahamika zaidi kama ‘Dogo Skillz’ ameambia TRT kuwa huzuni yake kubwa ni kuwa hangeweza kumpa mama yake zawadi aliyokuwa amempangia.

‘Mama ni kama nyota ya kun’gaa inayomulika maisha yako. Nawaomba muwatendee wema wangali wako nanyi,’’ Aliongeza Dogo Skillz, ambaye alifiliwa namama yake mwaka 2022.

Baadhi ya mashirika pia yalitumia fursa kuwatakia kina mama wanaofanya kazi nao hasa vikosi vya polisi na jeshi.

''Mama ndiye 'Gundi' anayeshikilia familia pamoja.'' Kikosi cha polisi Kenya kiliandika katika mtandao ya kijamii.

Ncini Uganda, Kikosi cha polisi kilitumia fursa hii kuwapongeza kina mama wanaohudumia wananchi, wakiwemo kina mama walioko sasa na walio staafu.

TRT Afrika