Huu ni mojawapo ya mikataba iliyosainiwa na mataifa hayo mawili katika kasri la Palais du Peuple, mjini Brazaville kwa lengo la kupanua ustawi wa kiuchumi baina yao, kuimarisha ushirikiano na kukuza biashara
Makubaliano hayo pia yanajumuisha ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, nishati, usalama, uzalishaji mafuta na ges imiongoni mwa zinginezo.
Akikaribisha kuondolewa kwa VIZA, Rais Ruto wa Kenya ametangaza kuharakisha ufunguzi wa ujumbe wa kidiplomasia mjini Brazzaville.
"Tuna nafasi kubwa ya kupanua kiwango, ukubwa na thamani ya shughuli za kibiashara kati ya mataifa yetu," Rais Ruto alisisitiza.
Ruto ameongeza kuwa Kenya imeanza mikakati ya kurejesha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Nairobi na Brazzaville huku akisisitiza kuwa uamuzi huo utaimarisha ushirikiano na kukuza biashara baina ya raia wa mataifa hayo.
Rais Ruto alisema nchi hizo mbili zimejitolea kutumia eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika AfCFTA ili kutumia vyema fursa za kibiashara zilizopo.
Kwa upande wake, Sassou-Nguesso amesema kuwa Kongo imejitolea kuimarisha biashara ya barani Afrika. "Tutatekeleza makubaliano haya kwa manufaa ya wananchi." Alisema.
Tangazo hilo limekuja baada ya kumalizika kongamano la wafanyabiashara wa mataifa hayo lililowaleta pamoja wawekezaji wa Kenya na Kongo, mjini Brazzaville
Djibouti, Comoro na Jamhuri ya Kongo ndizo nchi za hivi punde zaidi kuruhusiwa kuingia Kenya bila visa na utawala wa Ruto.
Rais Ruto amevalia njuga suala hili la kuondoa vikwazo vya usafiri kati ya nchi za Afrika kwa lengo la kuimarisha biashara ndani ya bara.