Msanii wa Nigeria Burna Boy alitumbuiza katika tuzo za Grammy za 2024. / Picha: Picha za Getty

Na

Charles Mgbolu

Shirika la Muziki yani "Academy" ya Kurekodi, waandaaji wa Tuzo za Grammy, imetangaza "Mkakati wa Upanuzi wa Kimataifa Afrika na Mashariki ya Kati."

Academy inasema ushirikiano huo ni na wizara za utamaduni na wadau muhimu kote Mashariki ya Kati na Afrika ili kuongeza juhudi zake za kusaidia watayarishaji wa muziki kwa kiwango cha kimataifa.

Lengo ni "kusaidia watayarishaji wa muziki kwa kiwango cha kimataifa kupitia rasilimali za kielimu zilizoboreshwa, kujifunza tamaduni tofauti, utetezi wa haki miliki, na zaidi," inasema Academy katika tangazo hilo.

Wizara za Utamaduni nchini Kenya, Ufalme wa Saudi Arabia (KSA), na Nigeria, Idara ya Utamaduni na Utalii huko Abu Dhabi kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), na Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni nchini Afrika Kusini zimetajwa kama washirika.

Makubaliano na mikataba pia zimesainiwa na Ghana na Ivory Coast, inasema.

Msaada kwa watayarishaji wa muziki

Academy inasema katika tangazo kuwa itawaunga mkono watayarishaji wa muziki katika ngazi zote, na kuwapa jukwaa na utetezi.

Itatoa mafunzo, programu za kielimu, na rasilimali zinazolenga mahitaji ya watayarishaji wa muziki katika maeneo haya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Academy ya Kurekodi, Harvey Mason Junior, ameitaja ushirikiano huo kama "wa kusisimua."

"Hii inasisimua kwa sababu muziki ni moja ya rasilimali kubwa zaidi za asili za wanadamu. Ni muhimu kuwa watu wanaojitolea kwa muziki wawe na msaada, rasilimali na fursa, bila kujali wanakotoka," Mason alisema.

Nyota mashuhuri wa Kiafrika kama vile Angelic Kidjo amepongeza tangazo hilo. Picha: Picha za Getty

Mwitikio wa Afrika

Upanuzi huo umepokelewa vizuri na wadau na wasanii wa Kiafrika.

"Rwanda inakubali maono haya ya kuunganisha akili za ubunifu za bara hili, ikionyesha wakati muhimu katika historia yetu ambapo utamaduni na roho yetu vinasherehekewa na kushirikiwa na dunia," alisema Francis Gatare, Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Maendeleo ya Rwanda.

Mwanamuziki mkongwe wa Afrika Angelique Kidjo alisema Afrika "iko tayari kwa mikono wazi."

"Academy ya Kurekodi inaharakisha juhudi zake za kuhudumia watu wa muziki kila mahali, na Afrika iko tayari kwa mikono wazi. Sisi ni bara la muziki na watengenezaji wa muziki vijana wenye shauku,'' alisema Kidjo.

Davido wa Nigeria alisema: "Kama mwanamuziki wa Kiafrika, ninashangazwa na upanuzi wa Academy ya Kurekodi katika Afrika na Mashariki ya Kati. Inatambua vipaji vyetu vya nguvu na ushawishi wa kimataifa wa muziki wa Kiafrika."

Mwaka huu, Grammy zilitambulisha kipengele cha kwanza cha Utendaji Bora wa Muziki wa Kiafrika, ambacho kinatambua rekodi zinazotumia maonyesho ya kipekee ya ndani kutoka kote barani Afrika.

TRT Afrika