Bunge la Wawakilishi wa Watu (HPR) lilifanya kikao cha kupitisha uamuzi kuhusu Tangazo la hali ya hatari. Addis Ababa / Picha: Reuters

Bunge la Wawakilishi wa Watu (HPR) la Ethiopia limeidhinisha rasimu ya tangazo la hali ya hatari katika jimbo la Amhara iliyoafikiwa na Baraza la Mawaziri mapema mwezi huu.

Kupitia kikao chake cha kwanza kisicho cha kawaida kilichoitishwa siku ya Jumapili, Bunge la taifa hilo liliipitisha rasimu ya tangazo hilo kwa kura nyingi baada ya kufanya majadiliano ya kina juu ya uamuzi huo na kuidhinisha huku 16 pekee wakipinga.

Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Tesfaye Beljige, aliwasilisha rasimu ya tangazo hilo na kufafanua kwamba mashambulizi yanayoungwa mkono na silaha yamefanywa katika eneo la Amhara na hali hiyo haiwezi kudhibitiwa na utekelezaji wa sheria mara kwa mara.

Tesfaye aliongeza kuwa vurugu za Amhara zimeikwaza serikali ya mkoa dhidi ya kutekeleza majukumu yake na kusisitiza umuhimu wa muswada huo kulinda nchi na kuwahakikishia wananchi amani na usalama.

Awali, serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwakamata washukiwa 23 na kuendelea kuwachunguza kuhusiana na ghasia katika eneo la Amhara.

TRT Afrika