Diamond alifanya biashara ya kuuza mitumba kabla ya kuanza kupanda majukwaani./Picha: Diamond

Mapenzi ya kazi yake, dhamira ya dhati ya kufikia mafanikio na kipaji ni baadhi tu ya sababu zilizomfanya msanii huyo kufikia viwango vya kimataifa.

Diamond, ambaye jina lake halisi ni Naseeb Abdul Juma, alizaliwa Oktoba 2, 1989 katika kata ya Tandale, jijini Dar es Salaam ambapo, maisha yake ya utotoni yalitawaliwa na changamoto za kutosha, hali iliyomlazimu, kwa kipindi fulani kuamua kuishi na bibi yake.

Sanura Kassim, maarufu kama Sandra ndiye mama mzazi wa msanii huyo.

Diamond Platnumz amejenga ukaribu na mama yake, na mara kwa mara wamekuwa wakifuatana./Picha: 

Diamond alipata elimu yake ya msingi kuanzia mwaka 1995 hadi 2002, na kumaliza elimu yake ya Sekondari mnamo mwaka 2006.

Ili kuweza kujikimu kimaisha, Diamond alijaribu kufanya shughuli kadhaa ikiwemo kuuza mitumba, kupiga picha mitaani na kufanya kazi katika kituo cha mafuta.

Hata hivyo, wakati wote huo, Diamond alikuwa na lengo moja tu, muziki. Kwa mujibu wa msanii huyo, ilimbidi kuuza pete ya mama yake ili apate pesa zitakazomuwezesha kuingia studio.

"Toka Mwanzo", ni wimbo wa kwanza wa Diamond, akiwa ameutoa mwaka 2006. Hata hivyo, ilimlazimu msanii huyo kusubiri miaka mingine minne kurekodi "Kamwambie", wimbo ulioupata umaarufu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Safari ya Diamond Platnumz ni kielelezo tosha cha uthubutu wake wa kufikia anga za kimataifa./Picha: Wengine

Katika wimbo huo, Diamond anamuomba rafiki yake kwenda kumueleza 'kipenzi chake cha zamani' kuwa bado anampenda na kumthamini, na kwamba asikubali kulaghaiwa na watu wenye pesa.

Wimbo wa "Kamwambie" ndio ulikuwa kama ufunguo kwenye mlango wa mafanikio ya Diamond, baada ya vigongo juu ya vigongo kama vile "Mbagala", "Nitarejea", "Mawazo", "Kesho", "Ukimuona", na zinginezo kufuata na kukonga nyoyo za mashabiki, wengi wakiwa wazungumzaji wa Kiswahili.

Nyota huyo wa muziki wa kizazi kipya Tanzania aliona haja ya kushirikiana na wasanii wengine kutoka bara la Afrika akiwa na azma ya kutanua wigo wa mashabiki wake.

Diamond Platnumz amefanya kazi kubwa kuhakikisha muziki wake unasambaa kila pembe ya dunia./Picha: Diamond Platnumz.        

Msanii kutoka Nigeria anayejulikana kama Davido ndiye aliyeanzisha safari ya muziki wa Diamond kuelekea Afrika ya Magharibi kipitia wimbo wa "Number One Remix". Wapo waliofuatia katika kufanikisha safari hiyo, akiwemo Flavour, Waje, Chike, Patoranking na wengineo.

Kwa upande wa kusini mwa bara la Afrika, Diamond alimshirikisha hayati AKA kupitia wimbo wa "Make Me Sing", na pia kufanikiwa kuliteka soko la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kufanya kazi na magwiji kama Papa Wemba na Koffi Olomide, ambaye alimshirikisha katika wimbo "Waah".

Msanii huyo kutoka Tanzania, amejizolea umaarufu kutokana na uwezo wake wa 'kunyambulika' , kwa uhodari na ujuzi anaouonesha jukwaani wakati anacheza, kuimba na hata kuisoma na kuelewa matakwa ya hadhira yake.

Mnyambuliko huu, ndio unamfanya pia ajikite kwenye biashara nyingine, zikiwemo studio ya kurekodi muziki na chombo cha habari.

Tayari, Diamond amekwishajikusanyia tuzo zisizopungua 30 katika safari yake ya muziki, ikiwemo ya MTV Europe na Channel O Music Video.

Msanii huyo ametwaa tuzo za kutosha katika tasnia ya muziki./Picha: Wengine

Awapo jukwaani, msanii huyo hujulikana kwa majina tofauti likiwemo la Chibu Dangote, ambalo limempatia umaarufu mkubwa kutokana na sifa za mtu tajiri kuliko wote barani Afrika, Mnigeria Aliko Dangote.

Ili upate huduma ya burudani kutoka kwa Diamond, basi itakupasa kumlipa kiasi cha kati ya dola za Kimarekani 70,000 hadi 100,000, kwa shoo moja.

Msanii huyo, ambaye utajiri wake unasadikiwa kufikia mamilioni ya dola za Kimarekani, ni baba wa watoto wanne kupitia wanawake tofauti.

Baadhi ya wanawake hao ni Zari Hassan kutoka Uganda, Mtanzania Hamisa Mobetto na Tanasha Donna Oketch kutoka Kenya.

TRT Afrika