Rekodi hiyo mpya, iliyo sawa na wimbo wake kuchezwa kwa dakika bilioni 1.5, imemfanya msanii wa kwanza wa kike mwenye nyimbo zilizotazamwa zaidi Afrika Mashariki.
Licha ya kuzama kwenye ulingo wa mziki takriban miaka mitatu iliyopita, baada ya kusainiwa na Wasafi, Zuchu amewapiku weledi waliomtangulia na kuwa kipenzi cha wengi haswa mashabiki wa mziki wa bongofleva ulio na mvuto zaidi kwa vijana ndani na nje ya Tanzania.
Rekodi hii inajiri baada ya kujizolea sifa hapo awali kwani kibao chake cha ‘Sukari’ kilikuwa kibao cha kwanza cha msanii wa kike kufikisha milioni moja ndani ya saa ishirini 22, alipoirusha hewani mnamo Januari 30, 2021.
Bado anashikilia rekodi ya msanii wa kike Afrika Mashariki mwenye wafuasi wengi kwenye YouTube, akiwa na wafuasi (subscribers) milioni 2.74 kufikia wakati wa kuandika ripoti hii.
Mnamo mwezi Machi 2021, msanii huyo wa lebo ya WCB aliandikisha rekodi nyingine kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kujizolea wafuasi million 1 kwenye YouTube.
Zuchu amewashukuru wasimamizi wake, wachezaji densi wake, waelekezaji wake, na waandalizi wake kwa kuchangia pakubwa ufanisi huo.
"Asanteni sana kwa pamoja tumeweza kufanikisha hii ndani ya miaka mitatu tumefikia hapaa."
"Hakuna video nimefanya bila dancers, namba pia zisingeongezeka bila bajeti, singeweza kufikisha lengo vizuru bila ya waelekezaji tungekosa kabisa content kali, bila ya producers ndo tusingekuwa na audio (sauti) kabisa, bila ya management (wasimamizi) tusingekuwa na nguvu hii tulionayo, bila mashabiki ndio kabisa mimi si kitu. Nasema asanteni sana kwa support. Alhamdulillah.
Zuchu sasa analenga kuvunja rekodi ya Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ambaye alitazamwa mara bilioni 2 kwenye YouTube na kuwa msanii wa kwanza Kusini ya jangwa la Sahara kufikisha idadi hiyo.