Kevin Philips Momanyi
TRT Afrika, Nairobi,Kenya
Zipporah Ong’era, 22 hajawahi kujua hisia za kutumia mikono yote miwili kufanya shughuli zake za kila siku. Alizaliwa bila mkono mmoja.
Licha ya ulemavu aliokuwa nao, anaamini sio kikwazo cha kumzuia kuishi maisha ya kawaida. Kupitia ujasiri aliokuwa nao, ameweza kutimiza ndoto zake, na hata kuwashinda ambao hawana ulemavu.
Uwezo wake umeshangaza wengi, hasa uamuzi wake wa kuamua kupika kwa kutumia mguu.
Utoto wake
"Nilipokuwa mtoto, nilitambaa kwa kutumia makalio. Ingawa kila kitu kilikuwa kigumu, lakini mama yangu hakuruhusu hali hiyo iniathiri kisaikolojia. Alinifundisha kukubaliana na hali yangu,’' anasema Zipporah.
Kuzaliwa na kukua katika mazingira ya bila mkono mmoja ilikuwa ni changamoto kwake hasa kutoka kwa jamii inayomzunguka.
Lakini mbaya zaidi, ni pale unyanyapaa ulipoanza ndani ya familia ambapo babake yake mzazi aliamua kuwakimbia na kuitelekeza familia kwa madai kwamba, kuzaliwa bila mkono mmoja ni laana.
‘’Nilipozaliwa, mama yangu aliambiwa kuwa mimi ni laana kwa familia na jamii. Mtoto aliyezaliwa na mkono mmoja tu alikuwa tofauti sana na hakuna mtu yeyote ambaye alikua amewahi kuona mtu wa aina hiyo. Nilipokuwa na umri wa miaka saba hivi, baba yangu naye alitukimbia. Mama yangu alijitahidi kunilea mwenyewe,’’anasema Zipporah.
Akimtaja mama yake kama chanzo kikuu cha msukumo wake chanya maishani, Zipporah alijifunza kutumia mguu wake kufanya kazi nyingi anazopaswa kufanya nyumbani.
‘’Naweza kufanya kila kitu pekee yangu. Ninaweza kupika, kusafisha, kufua na hata kulima shambani. Sijisikii tofauti na mtu yeyote yule kwa njia yoyote’’
Aliendelea na masomo yake na kuhitimu Shahada ya Sayansi ya Kompyuta. Hata hivyo, changamoto ilikuwa katika kupata kazi na zaidi kubahatika kuitwa katika usaili wake wa kwanza wa kazi.
Anakumbuka jinsi alivyopoteza nafasi hiyo ya kupata kazi baada ya mwajiri wake mtarajiwa kusema kwamba hangeweza kuifanya kazi kwa ufanisi kutoka na ulemavu wake.
‘’Naweza kufanya kila kitu pekee yangu. Ninaweza kupika, kusafisha, kufua na hata kulima shambani. Sijisikii tofauti na mtu yeyote yule kwa njia yoyote.’’
‘’Nakumbuka aliniuliza kama naweza kupiga chapa. Kati ya wote waliohojiwa, mimi pekee ndiye niliyeuliza hivyo. Sikuelewa kwa nini licha ya kuwa nimesomea kompyuta, aliamini kuwa siwezi kuitumia. Mwisho wa siku, ingawa ninaweza kupiga chapa vizuri, lakini sikupata kazi. Iliniuma sana, hata hivyo, haikunikatisha tamaa,’’ anasema Zipporah.
Ndoto ya maisha yake
“Ndoto yangu kuu ni kumpikia baba yangu chakula kwa kutumia mguu wangu. Natamani kumuonyesha uwezo niliokuwa nao licha ya kukosa mkono mmoja. Simchukii, nampenda. Mungu alimchagua kuwa baba yangu. Nina uhakika ipo siku atapata kuonja mapishi yangu," anasema.
Zipporah pia amehakikisha nuru yake inang'aa kwa wengine wenye kupitia changamoto kama zake. Hii ni kwa kupitia uchapishaji wa fulana ambazo huzigawa kwa watu wenye ulemavu.
Anasema anataka kuhamasisha mtu yeyote huko nje kama yeye kukumbatia makovu yao.
Fulana hizo zimeandikwa ujumbe maalumu, nao ni, ‘FLAWSOME’ ambao ni kifupi cha urembo, japo wenye makovu. Alama hii inaambatana na maneno ya Kihispania, ‘Sé tu propio tipo de hermosa’ aliyoyachora tattoo kwenye mkono wake wa kulia yenye maana, ‘Kuwa aina yako ya urembo.’
"Tatoo hii inanikumbusha kila siku kuwa mimi ni mrembo. Mama yangu ndiye mtu muhimu zaidi katika maisha yangu na amenitia moyo wa kujikubali. Ninaamini kuwa mimi ni mrembo na ninaishi kwa hilo. Bila mama yangu, sijui maisha yangu katika hii dunia yangekuaje,’'anasema Zipporah.
Zipporah anakiri kwamba, katika maisha, hakuna kitu kinachopatikana kwa njia rahisi.
“Kila mtu, hakosi kasoro, iwe ni ya kuonekana au ya kujificha. Ulemavu wa akili ndio kikwazo pekee ninachoamini ambacho kinaweza kumzuia mtu kufikia malengo yake," anasema.