Zambia, China zakubaliana kujenga kiwanda cha chanjo

Zambia, China zakubaliana kujenga kiwanda cha chanjo

Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kugharimu dola milioni 37.
Mradi huo utakuwa na tija kiuchumi, akiongeza kuwa hakutokuwa na urasimu wowote wakati wa utekelezaji wa mradi huo wa kuokoa maisha./Picha: HHichilema x.com

Zambia na China zimetiliana saini mkataba wa makubaliano wa ujenzi wa kiwanda cha kwanza kabisa cha kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu nchini Zambia.

Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kugharimu dola milioni 37, huku dozi milioni tatu zikizalishwa kupitia makubaliano kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza wakati wa kutiliana saini mkataba huo, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amesema hiyo ni hatua muhimu katika jitihada za kuondokana na magonjwa nchini humo, ambayo pia inaathiri nguvu kazi ya taifa hilo.

"Pia, tunatuma ujumbe kuwa Zambia, Afrika na dunia nzima kwa ujumla zinaweza kufanya kazi kwa pamoja. Ni lazima Zambia ichukuliwe kama mfano, kama kitovu cha uzalishaji kwa masoko makubwa. Hata ukiangalia, idadi ya watu barani Afrika inazidi kukua," alisema Hichilema kupitia televisheni ta taifa ya nchi hiyo.

Kulingana na Hichilema, mradi huo utakuwa na tija kiuchumi, akiongeza kuwa hakutokuwa na urasimu wowote wakati wa utekelezaji wa mkakati huo wa kuokoa maisha.

Ameongeza kuwa, mbali na kushiriki ujenzi wa kiwanda hicho, China itatoa msaada wa dozi milioni tatu za kipindupindu.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Afrika imeshuhudia ongezeko la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa mwaka 2024, hasa ukilinganisha na takwimu za mwaka 2022 ambapo wagonjwa 473,000 waliripotiwa na hiyo ilikuwa ni idadi mara mbili ya mwaka uliotangulia.

TRT Afrika na mashirika ya habari