Wakazi wakiondoka maeneo yaliyoathirika kwa mafuriko Maiduguri, kaskazini mwa jimbo la Borno, Nigeria, September 15, 2024. / Picha: Reuters

Zaidi ya watu 1,000 wamefariki na takriban 740,000 kukosa makazi huku mafuriko yakisambaratisha maeneo ya Afrika Magharibi na Kati, na kuathiri zaidi ya watu milioni 5 katika nchi 16, UN imesema.

Sehemu kubwa ya Afrika Magharibi na Kati pamoja na eneo la Sahel vimeshuhudia mafuriko makubwa na mvua nyingi.

Nchi za Chad, Niger, na Nigeria zimeathirika zaidi, zikiwa na zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya watu walioathirika, hayo ni kwa mujibu wa OCHA.

Mbali na athari za watu, maelfu ya nyumba, shule na vituo vya afya vimeharibika, pamoja na hekari nusu milioni za mashamba kuharibiwa, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula, hasa Chad na Niger.

Umoja wa Mataifa pia umetahadharisha kwamba hali mbaya ya maisha inaongeza uwezekano wa kuenea kwa magonjwa kama vile kama kipindupindu, katika nchi za Niger na Nigeria.

Joyce Msuya, msaidizi wa katibu mkuu wa masuala ya misaada na naibu mratibu wa msaada wa dharura, ametenga kiasi cha dola milioni 35 kusaidia Chad, Niger, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Congo. Hata hivyo, fedha zaidi zinahitajika, UN imesisitiza.

Nchini Nigeria pekee, Msuya ametenga dola milioni 5 kusaidia watu 280,000 kwa chakula, maji safi, na makazi, pamoja na jitihada za kuzuia kuibuka kwa kipindupindu.

Mpango wa msaada wa dola milioni 927 kwa Nigeria imedhaminiwa kwa asilimia 46 pekee, maafisa wamesema.

TRT World