Waokoaji wametoa zaidi ya miili 20 kutoka baharini nje ya kaskazini mwa Senegal baada ya boti iliyokuwa imejaa mamia ya wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanakwenda Ulaya kuzama, gavana wa jimbo na baadhi ya manusura wameiambia AFP.
"Zaidi ya miili 20 imepatikana," amesema gavana wa jimbo la Saint-Louis Alioune Badara Samb kwa simu Jumatano, na kuongeza kuwa wengine 20 wameokolewa.
Badara Samb hakusema ni abiria wangapi walikuwa kwenye boti lakini walionusurika wameiambia AFP kuwa idadi inaweza kufikia mamia.
Mamady Dianfo, kutoka Casamance kutoka pembezoni mwa kusini mwa nchi, amesema kulikuwa na takriban abiria 300 pindi boti lilipotoka Senegal wiki moja iliyopita.
Manusura mwengine, Alpha Balde, amesema abiria 200 walikuwa kwenye boti hiyo.
Pwani ya Senegal imekuwa ikitumika sana na wahamiaji na wakimbizi wa Kiafrika kuelekea bara la Ulaya kutafuta fursa za maisha.