Na Suleiman Jongo
Mabingwa wa soka nchini Tanzania , Young Africans wapo kambini wakijipanga kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya miamba ya Sudan, Al-Merreikh.
Mechi hiyo ya marudiano itachezwa Septemba 30 katika uwanja wa Chamazi, uliopo nje kidogo ya jiji kuu la biashara chini Tanzania, Dar es Salaam.
Yanga tayari ina mtaji wa magoli 2-0 ulioupata katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali iliyochezwa Kigali, Rwanda hivi karibuni, ambapo Al-Merreikh wameichagua nchi hiyo kama uwanja wake wa nyumbani, kufuatia hali tete ya usalama nchini Sudan.
Hivyo, vigogo hao wa Sudan wana kazi ya ziada kuhakikisha wanapata ushindi wa magoli 3-0 au kuendelea ili kuweza kufuzu hatua ya makundi.
Kocha wa Yanga raia wa Argentina, Miguel Gamondi amenukuliwa akisema kuwa hawatakubali itokee kupoteza mechi hiyo kwa sababu licha ya kuwa na uwezo wa kushinda, Yanga itakuwa uwanja wa nyumbani na kujivunia mtaji wa kutosha wa mashabiki wake.
“Tunahitaji ushindi ili kusonga mbele na hili ni moja ya malengo makubwa ya klabu,” amesema Gamondi.
Gamondi ana uzoefu wa soka la barani Afrika, akiwa na rekodi ya kufundisha vilabu kadhaa vikubwa barani Afrika kama vile Waydad Casablanca ya Morocco , CR Belouizdad ya Algeria, Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini na Esperance Sportiv de Tunis ya Tunisia, klabu aliyoitumikia alipokuwa kocha msaidizi mwaka 2004.
Kiu kubwa ya mashabiki wa Yanga ni kuiona klabu hii kongwe nchini Tanzania ikisonga mbele zaidi katika michuano ya kimataifa, baada ya msimu uliopita kufanikiwa kucheza fainali ya kombe la Shirikisho ilipokuwa chini ya kocha raia wa Tunisia Nassreddine Nabi, ambaye hivi sasa anaifundisha FAR Rabat ya Morocco.
Hata hivyo tayari Master Gamondi ameiteka mioyo ya mashabiki wa Yanga baada ya kuanza vizuri msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ukiwemo ushindi wa mwisho wa goli 1-0 dhidi ya Namungo na kukaa kileleni mwa ligi Kuu.
“Nimeweka mazingira kwa Yanga kuwa ni timu iliyo na uwiano mzuri katika kila idara, tazama tumeweza kufunga magoli mengi na kuruhusu goli moja tu katika michezo saba tuliyocheza, tena goli lenyewe ni la penati,” alinukuliwa Gamondi akisema hivi karibuni.
Maneno ya Gamondi kwa upande mwingine yanaonyesha kuwa Al-Merreikh, inayoathiriwa na vita nchini Sudan ambayo kwa zaidi ya miongo miwili haijawahi kufungwa na Yanga, ina kitu cha ziada cha kufanya kwa upande wao.
Inabidi wajipange vema kuikabili Yanga yenye nguvu zaidi ikiwa uwanja wa nyumbani na kupewa nguvu na wachezaji wanaopambania matokeo uwanjani.
Wachezaji wa Yanga wa kimataifa kama vile kiungo Aziz Ki kutoka nchini Burkina Faso, kipa Djigui Diarra kutoka Mali, mabeki wa pembeni Yao Attohoula (Ivory Coast), Joyce Lomalisa (Congo DRC), mabeki wa kati Gift Fred ( Uganda), viungo Pacome Zouzoua ( Ivory Coast ) na Khalid Aucho ( Uganda) kwa kushirikiana na wachezaji wazawa ndio wanaoifanya Yanga kuwa imara zaidi
Wengine ni pamoja na Mawinga ni Skudu Makudubela ( Afrika Kusini), Maxi Mpia Nzengeli, Jesus Moloko (Congo DRC), Kennedy Musonda (Zambia) na Hafiz Konkoni kutoka Ghana.
Hata hivyo, kocha wa Al-Merreikh Osama Nabieh amenukuliwa akisema kuwa timu yake haitakuja kinyonge Dar es Salaam na wapo tayari kupindua matokeo ya kigali kwa sababu mpira ni mchezo usiotabirika na dakika 90 ndio zinaamua matokeo.