Rais wa Kenya, William Ruto./Picha: TRT Afrika

Na Brian Okoth

Rais wa Kenya, William Ruto amesema kuwa muswada wa fedha uliokataliwa ulikuwa na manufaa mengi kwa nchi hiyo, licha ya kutafsiriwa vibaya na raia wengi.

Ruto, ambaye alizungumza katika mahojiano na vyombo vya habari vya nchi hiyo siku ya Jumapili, alisisitiza kuwa idara yake ya mawasiliano ilimuangusha kwa namna walivyofikisha ujumbe wa manufaa ya muswada huo kwa nchi hiyo.

Kulingana na Ruto, kitendo cha kuukataa muswada huo, kutairudusha nchi hiyo nyuma kwa "miaka miwili."

Laiti muswada huo ungekubaliwa na wengi, Ruto anaamini kuwa nchi hiyo ingekuwa na uwezo wa kujitegemea katika bajeti yake yenyewe, kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kufanya majadiliano

Mbali na mambo mengine, muswada huo ulilenga kuongeza ushuru kwenye huduma mbalimbali kama vile pedi za kike, simu za mikononi na pikipiki.

Wakati huo huo, muswada huo pia ulilenga kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye vifaa vya ujenzi, hospitali na zingine katika sekta ya utalii.

Maandamano ya hivi karibuni yalianza kwa amani lakini yaliishia na vurugu zilizoshuhudia sehemu ya jengo la Bunge la taifa likichomwa moto.

'Kazi kubwa ya kuitoa Kenya kwenye mzigo wa madeni'

Rais Ruto alisitisha zoezi la kusaini muswada huo kuwa sheria, kufuatia vurugu hizo.

Alirudisha muswada huo bungeni ili baadhi ya vipengele viweze kuondolewa.

"Tumetupilia mbali muswada wa sheria. Hii inamaanisha kuwa tunarudi nyuma kwa miaka miwili. Inamaanisha kuwa mwaka huu, tutakopa dola bilioni 7.7 ili kuendesha serikali yetu," Ruto aliongeza.

"Nimekuwa nikifanya kazi ya ziada kujaribu kuiondoa Kenya katika mzigo wa madeni. Ni vyema tukaweka muswada huu katika muktadha. Ni rahisi sana kusema kuwa tunakataa kama nchi. Ni vyema. Nami, kwa moyo mweupe nikakubali, lakini ni uamuzi utakaokuwa na athari kubwa sana."

"Nina kazi ya kufanya"

Ruto aliongeza kuwa Kenya imekusanya mapato yanayofikia dola bilioni 17.8 katika mwaka wa fedha 2023/2024 , lakini dola bilioni 9.3 zilitumika katika kulipa madeni na kulipa mishahara ya wafanyakazi wa serikalini.

Kumekuwepo na shiniko la kumtaka Rais Ruto ajiuzulu kufuatia maandamano ambayo yamesababisha vifo vya watu 23 na mamia kujeruhiwa, kulingana na Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR).

Hata hivyo, Rais Ruto anasisitiza kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha katika maandamano hayo ni 19 tu.

Kuhusu shinikizo la kujiuzulu, Rais Ruto alisema kuwa "bado ana kazi ya kufanya" na kuwa hayuko tayari kujiuzulu lakini anaheshimu uhuru wa kujieleza kati ya Wakenya wote.

'Uharibifu wa mali'

Kulingana na Ruto, mali zenye thamani ya dola milioni 18.6 ziliharibiwa wakati wa maandamano hayo ya wiki mbili.

Licha ya kuanza kwa hali ya amani, Ruto anasema kuwa baadhi ya magenge ya wahuni walitumia mwanya wa maandamano kufanya uhalifu, na kuwalazimu "jeshi la polisi kutumia nguvu."

Alipoulizwa kuhusu namna ya polisi walivyouwa baadhi ya waandamani, Ruto alisema: "Polisi wana maelezo ya kutoa kutokana matendo yao."

"Hakutakuwa na mauaji ya kiholela nchini Kenya, nimetimiza ahadi yangu," aliongeza.

"Matukio ya utekaji"

Kuhusu ongezeko la hivi karibuni la matukio ya utekaji nyara unaoongozwa na polisi, haswa kwa watu wanaodhaniwa kuwa wanapinga sera za serikali, Ruto alisema: "Ikiwa kuna watu waliokamatwa (kufanywa) na polisi, (hao) si utekaji nyara ."

"Ikiwa Polisi wamekuita kituoni kwao na wewe ukaamua kugoma, haalfu waje kukumata, je, huo ni utekaji?" alihoji.

Wiki ijayo, baadhi ya Wakenya wamesema kuwa watashiriki katika maandamano ili kushinikiza kujiuzulu kwa Rais William Ruto ambaye pia, serikali yake iliamua kutumia jeshi ili kukabiliana na waandamanaji.

Rais anasema jeshi litatumika kudhibiti maandamano "kama hatua ya mwisho."

Kupunguzwa kwa bajeti

“Polisi watakuwepo kuhakikisha kwamba wahalifu wanashughulikiwa,” Ruto alisema.

Katika mwaka mpya wa kifedha, Kenya italazimika kufanyia kazi bajeti yake kulingana na Sheria ya Fedha iliyopo tayari ya 2023 ambayo ilichota bajeti ya shilingi dola bilioni 28.6 kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Kupitia muswada uliokataliwa, Kenya imechota bajeti ya dola bilioni 30.1 kwa mwaka mpya wa fedha.

Rais Ruto alisema serikali yake italazimika kuchukua hatua za kubana matumizi.

TRT Afrika