Rais wa Liberia George Weah amekubali kushindwa na mpinzani wake Joseph Boakai, makamu wa rais wa zamani, katika uchaguzi wa marudio uliokuwa na ushindani mkali nchini Liberia.
Boakai alishinda 50.89% ya kura huku karibu 99.58% ya vituo vya kupigia kura vimehesabiwa, kulingana na matokeo ya uchaguzi wa Novemba 14 ambayo yalitangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Davidetta Browne Lansanah siku ya Ijumaa. Weah alipata 49.11% ya kura.
"Matokeo yaliyotangazwa usiku wa leo, ingawa sio ya mwisho, yanaonyesha kuwa Balozi Joseph Boakai yuko kwenye uongozi ambao hatuwezi kuupita. Kwa hivyo, dakika chache zilizopita, nilizungumza na Rais mteule Joseph Boakai kumpongeza kwa ushindi wake,” Weah aliambia taifa.
"Tunapokubali matokeo, tutambue pia kwamba washindi wa kweli wa uchaguzi huu ni watu wa Liberia," alisema.
"Umeonyesha tena kujitolea kwako kwa kanuni za kidemokrasia zinazotuunganisha kama taifa. Watu wa Liberia wamezungumza na tumesikia sauti yao,” aliongeza.
Msingi wa pamoja
Weah alikiri kuwa kinyang'anyiro hicho kikali kilifichua mgawanyiko mkubwa nchini.
"Tunapohamia utawala mpya, lazima tuwe macho dhidi ya hatari za mgawanyiko, na lazima tushirikiane kutafuta muafaka. Sasa, zaidi ya hapo awali, lazima tushikane kwa upendo wa Mama Liberia,” alisema.
Kura hiyo ya marudio ilifanyika baada ya kushindwa hata mmoja wa wagombea kupata alama zaidi ya 50% zinazohitajika kushinda duru ya kwanza ya upigaji kura Oktoba.10.
Katika duru hiyo ya kwanza, Weah alipata 43.83% ya kura huku Boakai, kutoka chama cha upinzani cha Unity Party, akipata 43.44%.
Serikali ya kujumuisha wote
Boakai, 78, alihamasisha vyama vya upinzani kumuunga mkono "kulikomboa taifa kutoka kwa utawala ulioshindwa unaoondoka madarakani ukiongozwa na Rais Weah."
Boakai alihudumu kama makamu wa rais kutoka 2006 hadi 2018 chini ya Rais wa zamani Ellen Johnson Sirleaf.
Aliahidi kuunda serikali ya ushirikishwaji ambayo inaakisi kweli tofauti za kisiasa, kijamii na kidini za wananchi.
Wawili hao walishindana katika duru ya pili ya upigaji kura katika uchaguzi wa 2017 ambapo Boakai alimfuata Weah katika duru ya kwanza. Weah, 57, alishinda 60% katika kura ya awamu ya pili ya 2017.