Aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya kale Zanzibar, Simai Mohamed Said akizungumza katika tamasha la Utalii la SITE./Picha: TRT Afrika.              

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Waziri wa Utalii na Mambo ya kale wa Zanzibar, Simai Mohamed Said amejiuzulu.

Kulingana na picha mjongeo zilizosambazwa na Simai mwenyewe, mwanasiasa huyo alisema kuwa amemwandikia Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi barua hiyo ya kujiuzulu, huku akilalamikia mazingira yasiyo rafiki katika utekelezaj wa majukumu yake ya kila siku.

"Nimefikia uamuzi huu ambao ni mgumu kwa utamaduni kwa Kizanzibari, kutokana na imani yangu kuwa jukumu namba moja la wasaidizi wa Rais, wakiwemo mawaziri ni kumsaidia katika kutekeleza ilani ya chama tawala na ikitokea mazingira yasiyo rafiki katika kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa ustawi wa wananchi, ni vyema kutafuta jawabu kwa haraka ili kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo iweze kuendelea, na hata ikibidi kukaa pembeni," amebainisha Simai, ambaye pia ni mwakilishi wa jimbo la Tunguu kupitia CCM.

Kwa upande wake, katika taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena A. Said, imesema Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amekubali ombi la kujiuzulu kwa Simai Mohammed Said, kuanzia tarehe 26, Januari, 2024.

Simai aliteuliwa kama Waziri wa Utalii na Mambo Kale mwezi Machi mwaka 2022, akitokea katika nafasi ya Naibu waziri wa Elimu aliyoipata mwaka 2019.

Siku chache zilizopita, wakati akizungumza na wadau wa utalii Zanzibar, Simai alisikitishwa na maamuzi ya Bodi ya vileo Zanzibar iliyosababisha upungufu mkubwa wa bidhaa hizo kwenye hoteli za kitali visiwani humo.

Kulingana na Simai, maamuzi ya bodi hiyo ya kuwabadilisha wasambazaji wa vileo kutoka Tanzania bara na nje ya nchi, bila kuwashirikisha wadau wa utalii visiwani humo, kuliathiri uendeshaji wa sekta hiyo.

"Inakuwa sio vyema maamuzi kufanywa na taasisi nyingine bila sisi huku hatujajitayarisha kwani inaleta madhara makubwa sana kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi," alisema.

Takribani asilimia 30 ya pato la visiwa hivyo linatokana na sekta ya utalii.

TRT Afrika