Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly atakutana na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta, mjini Kigali. Picha Reuters

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza James Cleverly atakutana na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta, mjini Kigali Jumanne asubuhi, kutia saini mkataba mpya wa kuwatuma wasaka hifadhi hadi taifa hilo la Afrika.

Chini ya mpango huo, Uingereza inakusudia kuwapeleka Rwanda, maelfu ya waomba hifadhi ambao walifika pwani yake bila ruhusa, katika jitihada za kuwazuia wahamiaji wanaovuka bahari kwenda Ulaya kwa boti ndogo.

"Rwanda inajali sana haki za wakimbizi, na ninatarajia kukutana nao kutia saini makubaliano haya na kujadili zaidi jinsi tunavyofanya kazi pamoja kukabiliana na changamoto ya kimataifa ya uhamiaji haramu," Cleverly alisema.

Rwanda imepokea malipo ya awali ya pauni milioni 140 (Dola180 milioni) kwa ahadi ya pesa zaidi za kufadhili malazi na utunzaji wa watu wowote waliohamishwa.

Ziara ya Cleverley inajiri baada ya mahakama ya juu ya Uingereza kutangaza mpango huo wa uhamisho kuwa kinyume cha sheria.

Ukiukaji wa sheria za kimataifa

Mpango wa Rwanda uko katikati ya mkakati wa serikali wa kupunguza uhamiaji na unatazamwa kwa karibu na nchi zingine zinazozingatia sera kama hizo.

Hata hivyo, mwezi uliopita, mahakama kuu ya Uingereza iliamua ndege hizo zitakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu zilizowekwa katika sheria za ndani.

Mahakama kuu iliamua mpango wa serikali wa kutuma waomba hifadhi nchini Rwanda ulikuwa kinyume cha Sheria kwa sababu kulikuwa na hatari kwamba wakimbizi waliohamishwa hawangepata mazingatio yao kihalali au kurudishwa nchi zao za asili ili kukabiliwa na mateso.

Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak yuko chini ya shinikizo kubwa la kupunguza uhamiaji, ambao uligonga rekodi ya watu 745,000 mwaka jana, na kumaliza mtiririko wa wanaotafuta hifadhi ambao hulipa wasafirishaji wa watu kwa njia zao hatari za kuvuka, mara nyingi katika boti zilizojaa, zisizofaa baharini.

Mpango huo wa uhamiaji wa Rwanda ulitangazwa na Waziri mkuu wa zamani Boris Johnson mwaka jana, lakini hakuna mtu anayetafuta hifadhi aliyetumwa nchini humo.

Reuters