Waziri wa Nchi anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano ya Viwanda wa Uganda, Kanali (mst) Charles Okello Engola ameuawa kwa kupigwa risasi asubuhi ya leo na mlinzi wake kutoka nyumbani kwake Kyanja, kitongoji cha Kampala.
Spika wa Bunge, Bi Anita Among, alithibitisha kifo cha waziri huyo alipokuwa akiongoza kikao cha bunge leo asubuhi.
“Leo asubuhi, nilipata taarifa za kusikitisha kuwa Mhe Engola amepigwa risasi na mlinzi wake na baada ya hapo mlinzi akajipiga risasi yeye mwenyewe. Roho yake ipumzike kwa amani. Huo ulikuwa mpango wa Mungu. Hatuwezi kubadilisha chochote,” Bi Among alisema.
Msemaji wa Polisi Uganda, Fred Onanga, alithibitisha kisa hicho kupitia maongezi na waandishi wa habari akisema "Waziri huyo aliuawa kwa kupigwa risasi mwendo wa saa nane asubuhi alipokuwa akiingia kwenye gari lake kwenda kazini."
"Mlinzi alikimbia akaingia katika kinyozi moja mtaani akajipiga risasi." alisema huku akisisitiza kwamba uchunguzi unaendelea na hawataki kutaja kwa sasa sababu zilizompeleka mlinzi huyo kumuuwa Waziri.