Pendekezo hilo ni mojawapo ya maafikiano ya kamati ya mazungumzo ya kitaifa ya wanachama kumi - inayoitwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) baada ya miezi minne ya mashauriano kati ya wawakilishi wa mrengo unaotawala na ule wa upinzani.
Kwa mujibu kamati hiyo Waziri mkuu Kenya atateuliwa na rais , na baadaye kuidhinishwa na bunge la Taifa.
Raila Odinga ndiye alikuwa waziri mkuu wa mwisho wa Kenya alipohudumu kutoka 2008 hadi 2013.
Raila Odinga alichukua cheo hicho mwishoni mwa mazungumzo ya kitaifa ya maridhiano nchini humo yaliyoongozwa na Kofi Annan Februari 2008.
Aliyekuwa rais wa wakati huo, Mwai Kibaki na Raila Odinga, walisaini mkataba wa amani wa Taifa ulirejesha utulivu nchini humo kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 na zaidi ya watu 600,000 kuachwa bila makao kati ya 2007/2008.
Kibaki na kinara wa upinzani Raila Odinga walikuwa chini ya shinikizo la kufikia suluhisho la haraka kufuatia mapigano ya baada ya uchaguzi. Mazungumzo hayo yalidumu zaidi ya mwezi mmoja kutokana na kutoelewana kati ya wakuu hao wawili na mirengo ya ODM na PNU.
Mbali na kurejeshwa kwa cheo cha Waziri mkuu, ofisi ya kiongozi mkuu wa Upinzani pia imependekeza kurudishwa rasmi.
Jopo la mazungumzo ya kitaifa lililoongozwa na wenyekiti Kalonzo Musyoka wa muungano wa upinzani wa Azimio na Kimani Ichung'wa wa mrengo unaotawala wa Kenya Kwanza.
"Tumeiweka Kenya mbele ya matamanio ya kibinafsi, tukitambua kuwa umoja wa watu wetu na ustawi wa taifa letu ni muhimu," wawili hao walisema kwa kauli moja.
Aidha, kamati hiyo iliyokuwa na wanachama 10, pia imehoji kuwa uundaji wa ofisi hizo mbili zitakuza uwiano na maaridhiano kati ya pande mbili za upinzani na serikali.
"NADCO inapendekeza kuanzishwa kwa Ofisi ya Kiongozi rasmi wa upinzani, ambaye ni kiongozi wa chama kikubwa/ muungano wa vyama vya siasa ambavyo vilipata idadi kubwa ya kura katika uchaguzi wa rais uliotangulia na manaibu wawili," taarifa ilisema.
Miongoni mwa mapendekezo mengine, ni uundwaji wa tume huru ya udhibiti wa vyama vya siasa.
"Pazia la NADCO linapokunjwa, na nchi ikiendelea na safari yake ya kujenga taifa, ilikuwa ni heshima kwa wanaume na wanawake wote katika chumba hiki, ambao waliitwa kuchukua hatua na kuitumikia nchi hii katika saa yake ya uhitaji. Kamati hiyo ilimaliza.